habari Mpya


Wafungwa 713 Waachiwa Huru Kagera.


Na: Sylvester Raphael.

Wafungwa waliopata msamaha wakiongozwa na Marwa Maganya walimshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kuwasamehe na kuwatoa gerezani wengi wao wakikiri kujutia makosa yao yaliyowapeleka kifungoni na kuwaasa wananchi ambao hawajawahi kufungwa kutojihusisha na masuala ya uvunjifu wa sheria kwani Gerezani si mahala pazuri, aidha waliwasisitiza wananchi kuchapa kazi kuwa usipofanya kazi ukiwa uraiani ukipelekwa gerezani utafanyishwa kazi hizo kwa nguvu bila kujali unataka au hutaki.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti amesimamia utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli alilolitoa Desemba 9, 2019 katika sherehe za miaka 58 ya uhuru na 57 ya Jamhuri baada ya kutoa msamaha kwa wafungwa nchini na kuagiza utekelezaji kufanyika mara moja bila kucheleweshwa huku mkoa wa Kagera ukiongoza kwa wanufaika wa msamaha huo 713.

Mkuu wa Mkoa Gaguti katika kutekeleza agizo hilo alifika Gerezani la Kitengure Wilayani Karagwe, kusimamia na kuhakikisha agizo la Rais Magufuli linatekelezwa bila kucheleshwa kwani Geraeza la Kitengule ndilo lilikuwa linaongoza kwa kuwa na wafungwa wengi 256 waliopata msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani kati ya Magereza nane yaliyomo Mkoa ni Kagera.
“Nimefika hapa Gerezani Kitengule kuhakikisha ninyi nyote mliopata msamaha jana mnatoka mapema kama Mhe.Rais Magufuli alivyoelekeza na kufikia jioni ya leo tutakuwa tumepata picha kamili ambayo itaonesha wafungwa wote 713 katika mkoa kuwa wametolewa ndani. Najua mliokuwa Gerezani tayari mmejutia makosa yenu na mnaporejea uraiani mnatakiwa kuchapa kazi kwa nguvu tukaijenge nchi yetu kwa pamoja, kwa niaba ya Mhe. Rais nawatakia heri mkachape kazi mkajiletee maendeleo yenu mmoja mmoja na taifa kwaujumla”. Aliwaasa Mhe Gaguti.
Kwa mujibu wa Afisa Mnadhimu Namba Moja wa Magereza Mkoa wa Kagera Kamishina Msaidizi Mtemi S. Kasolwa, Wafungwa waliopata msamaha mkoa wa Kagera jumla ni kutoka katika Magereza nane ambayo ni, Gereza la Bukoba Wafungwa 101, Muleba wafungwa 65, Ngara wafungwa 35, Rusumo wafungwa 55, Kitengule wafungwa 256, Kayanga wafungwa 71, Biharamulo wafungwa 83 na Rwamurumba wafungwa 47 na kukamilisha jumla ya wafungwa 713.

Aidha, Kamishina Msaidizi Mtemi alisema kuwa idadi hiyo ni kubwa kwasababu baadhi ya wafungwa wanahamishwa kutoka mikoa mingine kuletwa mkoani Kagera kwaajili ya kutumikia vifungo vyao mfano Gereza la Kitengule ambalo ni gereza la kilimo ambalo linapokea wafungwa kutoka mikoa mingine kwa ajili ya uzalishaji.

Post a Comment

0 Comments