habari Mpya


Kahawa Yaipatia Tanzania Sh 283.7 Bilioni.

Serikali ya Tanzania imesema mauzo ya kahawa katika msimu wa mwaka 2018/2019 yamewezesha kuliingizia Taifa dola za Marekani milioni 123 sawa na takriban Sh283.7 bilioni.

Naibu Waziri wa Kilimo, Bw.Omary Mgumba aliyekuwa akizungumza (Novemba 12, 2019) Bungeni amesema hadi kufikia mwisho wa msimu wa 2018/2019 kiasi cha tani 66,646 cha kahawa kiliuzwa ikiwa ni asilimia 102.8 ya makisio ya uzalishaji wa tani 65,000.

Kati ya tani hizo zilizouzwa, tani 41,971 zimeuzwa kupitia minada ya kahawa na 24,575 zimeuzwa katika soko la moja kwa moja,” amesema Bw.Mgumba. 

Mauzo hayo yaliwezesha kuliingizia Taifa takriban Sh283.7 bilioni yakiwa yameshuka ikilinganishwa na msimu wa 2017/2018 ambapo mauzo yalikuwa Sh341 bilioni

Huenda mapato yatokanayo na uuzaji wa kahawa yakaendelea kupungua hata katika msimu wa mwaka 2019/2020, baada ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kusema uzalishaji wa zao hilo utashuka kutokana na mzunguko mdogo na kuchelewa kwa mvua katika mikoa ya kanda ya kaskazini ikiwemo Kilimanjaro na Arusha.

Katika taarifa ya Hali ya Sekta ya Kahawa Tanzania iliyotolewa na TCB mwezi April 2019 inaeleza kuwa matarajio ya uzalishaji wa kahawa katika msimu ujao wa 2019/2020 yatakuwa tani 50,000 ambapo ni sawa na upungufu wa asilimia 23.6 ukilinganishai na uzalishaji wa mwaka  2018/2019.

Aidha, Serikali imewahakikishia wakulima wa kahawa nchini kuwa mifumo ya mauzo ya moja kwa moja pamoja minada katika mikoa ya Kilimanjaro na Songwe, Ruvuma, Njombe, Kagera inayotumika msimu wa 2019/2020 itaendelea kutumika nchini.

Post a Comment

0 Comments