habari Mpya


DC Kibondo- ‘’Shiriki Kutokomeza Malaria Kabisa kwa Manufaa ya Jamii’’.

Na James Jovin – RK Kibondo.

Zoezi la upuliziaji dawa ya ukoko majumbani litakalogharimu zaidi ya shilingi  bilioni Nne limeanza katika wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ikiwa ni mikakati ya Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kuhakikisha ugonjwa wa Malaria unatokomezwa.

Zoezi hilo linalotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la ABT Associate chini ya Ufadhili wa Serikali ya Watu wa Marekani  limezinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Kibondo Bw. Luis Bura ambapo katika mkoa wa Kigoma zoezi hilo linafanyika katika wilaya za Kibondo,Kasulu na Kakonko.
Bw. Bura amesema kuwa zaidi ya nyumba 70,000 zitafikiwa na zoezi hilo katika wilaya ya Kibondo ambapo zoezi hilo lililoanza rasimi October 23, 2019 litafanyika pia katika Kambi ya Wakimbizi Nduta.
Baadhi ya Wananchi waliozungumza na Redio Kwizera wamelipokea zoezi hilo kwa mikono miwili kwa kuwa dawa hiyo itasaidia kupunguza ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa tishio hasa kwa akina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa wilaya ya Kibondo Dr. Pima Sebastian amesema kuwa kiwango cha Malaria katika wilaya ya Kibondo kimefikia asilimia 25.8 hivyo amewataka Wananchi kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo ili kusaidia kupunguza ama kumaliza kabisa ugonjwa wa Malaria.

Post a Comment

0 Comments