habari Mpya


RC Kagera- 'Hatuna Changamoto Fedha za Malipo ya Awali Kwa Wakulima wa Kahawa'.

Na: Sylvester Raphael – Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti afanya ziara katika wilaya tatu kukagua msimu wa kahawa wa 2019/2020 unavyoendelea hasa lengo kuu likiwa ni kuona wakulima kama wanalipwa fedha zao kwa wakati bila ucheleweshwaji na kama kuna changamoto zozote ziweze kutatuliwa.

Septemba 3, 2019 Mhe. Gaguti akiwa katika Chama cha Msingi Muungano na Nkwenda Wilayani Kyerwa, akiongea na wananchi na wakulima wa kahawa alisema kuwa taarifa alizonazo na anazozipokea kila siku ni kuwa Vyama Vikuu vya Ushirika vya KDCU LTD na KCU 1990 LTD havidaiwi na Vyama vya Msingi kwa hiyo hakuna sababu ya malipo ya kwanza kwa wakulima kucheleweshwa.
Ukiondoa wakulima ambao walipeleka kahawa zao kwenye vyama vya msingi ndani ya siku saba hadi kumi kufikia leo tarehe 3 Septemba, 2019 wakulima wote hakuna anayedai kwani fedha zipo za kuwalipa, taarifa nilizonazo hakuna mkulima yeyote anayedai fedha za mwezi wa saba mwisho wa kulipa ilikuwa ni tarehe 23.08.2019.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti

Katika Vyama vya Msingi vya Muungano, Nkwenda Wilayani Kyerwa na Kamahungu Wilayani Karagwe akiongea na wakulima Mhe. Gaguti alitoa nafasi kwa wakulima wanaovidai Vyama vya Msingi malipo ya kwanza ya muda mrefu kujitokeza ili ajue tatizo ni nini. 

Katika mikutano hiyo wakulima waliojitokeza ni wale ambao walipeleka kahawa zao kwenye vyama vya msingi mwishoni mwa mwezi wa Agosti, 2019 na malipo yao tayari yapo kwa taratibu za kulipwa tangu tarehe 3/08/2019.
Aidha, Mhe. Gaguti alimchukulia hatua za kinidhamu mkulima mmoja wa Chama Msingi Kamahungu Wilayani Karagwe kwa kumdanganya kuwa anadai chama hicho fedha zake tangu mwezi Julai 2019 ambapo alipohakiki katika vitabu vya chama hicho alikuta kuwa si kweli mkulima yule aliuza kahawa yake mwezi Julai bali mwishoni mwa mwezi Agosti 2019.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa bado hajaridhishwa na matumizi ya ushuru unaokatwa kwenye kahawa ya wakulima na Vyama vya Msingi ambapo alisema kuwa tayari analifanyia kazi suala hilo kuona ushuru huo unapunguzwa na mkulima anapata fedha zaidi maana fedha hiyo inatumika bila ridhaa ya wakulima wa Vyama vya Msingi bali viongozi vinatumia fedha hizo na kutoa taarifa kwa wakulima jambo ambalo si sawa.
Katika suala hilo Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa angependa kuona fedha za ushuru zinaboresha kwanza Vyama vya Msingi kuliko kwenda kwenye matumizi mengine. Fedha hizi zingeweza kununulia mizani ya kidigitali ambayo itaondoa utata katika upimaji wa kahawa ya mkulima, pili fedha hiyo inunue vifaa vya kupima unyevunyevu katika kahawa ili mkulima asiendelee kukatwa kilo moja ya unyevu kwenye kahawa yake.

Hili tunalifanyia kazi na nitaunda timu ya wataalam ili kuhakikisha changamoto zote hizo katika zao la kahawa linapatiwa ufumbuzi na mkulima kuneemeka na jasho lake.” Alisistiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Katika Wilaya ya Missenyi, Mhe. Gaguti alitembelea vitalu vya kuzalisha miche ya kahawa ambapo lengo ni kuinua uzalishaji katika Wilaya hiyo.

Katika msimu wa mwaka huu wa kahawa wa 2019/2020 tayari Vyama Vikuu vya Ushirika vya KCU 1990 LTD na KDCU LTD mkoani Kagera vimekusanya zaidi ya kilo milioni 35 sawa na asilimia 75 ya kahawa inayotarajiwa kukusanywa katika msimu mzima na zaidi ya shilingi bilioni 35 tayari zimelipwa kwa wakulima. Aidha, makisio ya ukusanyaji katika msimu huu ni kukusanya kilo milioni 52.

Post a Comment

0 Comments