habari Mpya


Msimu wa Vuli uwe Kipimo Bora kwa Mitaro Mipya.

MSIMU wa Mvua za vuli umeanza na Mamlaka  ya hali ya hewa Tanzania (TMA) imeeleza kuwa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka huu , 2019 yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (mvua za vuli).

Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, alisema kuwa mvua hizo  ni kwa maeneo mahususi ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Dk. Kijazi, alisema kuwa katika msimu wa mvua wa vuli mwaka huu, maeneo mengi ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki pamoja na Pwani ya Kaskazini yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani, hadi chini ya wastani, pamoja mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika ameneo ya ukanda wa ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Aidha alisema maeneo machache ya mkoa wa Kagera mvua za nje ya msimu zinaendelea toka mwezi Agosti na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine ya ziwa Victoria hadi kufikia wiki ya pili ya mwezi Oktoba, hivyo kuungana na msimu wa mvua za vuli.

Alisema kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyangakatika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba.

Alifafanua kuwa msimu wa mvua za vuli katika maeneo yanayotarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari mwaka 2020.

Alieleza kuwa ukanda wa Pwani ya kaskazini ,mikoa ya DAR ES Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, ambapo katika maeneo hayo kunatarajiwa kuanza mvua katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu.

Alisema vipindi virefu vya ukavu na mvua chache pia vinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani ya kaskazini, hata hivyo mvua zinatarajiwa kunyesha kiwango cha wastani kuanzia wiki ya pili ya mwezi Novemba, ambapo maeneo hayo kunatarajiwa kuisha mvua katika wiki nne ya mwezi Disemba.

Aliongeza kuwa mvua katika maeneo ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Octoba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya waastani katika meneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, ambapo mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba mwaka huu.

Hata hivyo, alitoa tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali kama kilimo na usalama wa chakula, mifugo na wanyama pori, maliasili na utalii, nishati na maji, mamlaka za miji, afya pamoja  na menejimenti za maafa.

Matokeo hayo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, nafikiri ni wakati muafaka wa kujiandaa kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza katika kipindi hiki cha angalizo kwa vile ni muhimu kwa jamii kuufuata utabiri huu, ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza katika msimu huu wa mvua za vuli.

Hili ni jambo la msingi kutokana na kwamba madhara ya mvua huwa hayapigi hodi, ila hujitokeza pale inaponyesha na matokeo yake huwa makubwa kiasi ambacho kinga yake huwa ni ndogo sana.

Leo hii, si jambo la ajabu kuona madhara ya mafuriko yanakuwa makubwa jambo ambalo limeifanya serikali kutoa tahadhari kila wakati, na huku ikijiandaa kufungua kambi za kuzuiya maafa yasiwe makubwa katika maeneo yanayokumbwa na matatizo.

Inafurahisha hivi sasa serikali ya Zanzibar imejikita katika utengezaji wa mitaro mipya ya kupokelea maji ya mvua jambo ambalo litahitajika kwa jamii kuona umuhimu wa kuitumia vyema ili iweze kufanya kazi vyema.

Hili ni jambo la msingi kutokana na hivi sasa kuwepo kwa tabia ya baadhi ya watu kutumbukiza taka katika mitaro kama vile ni jambo la kawaida, kiasi ambacho huifanya kushindwa kufanyakazi zake sawasawa.

Hii ni kutokana na kuigeuza mitaro ya kupitishia maji taka kuwa ndo majaa makubwa ya uchafu utokao majumbani kiasi ambacho huifanya kuziba na kusababisha maji kushindwa kufuata mkondo wake.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa Mamlaka zilizotajwa katika utabiri huu zinapaswa kujiandaa kuzuiya athari zisiwe kubwa kwa vile ni jambo lolilozoeleka kuona kunakuwa na kinga kuliko kutibu.

Post a Comment

0 Comments