habari Mpya


Shindano la Usafi wa Mazingira Mwaka 2019 Tanzania, Kushirikisha Halmashauri 184.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile.

Na Frank Mvungi

Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2019 kushirikisha Halmashuri zote 184 Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari June 12,2019 Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa tarehe ya kuanza kwa mashindano hayo itatajwa hivi karibuni ambapo Halmashauri zitakazoshinda ngazi ya mkoa zitashindanishwa Kitaifa.

Katika mashindano hayo Wizara imeongeza vipengele viwili ambavyo ni Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa na Taasisi za kibenki kwa kila mkoa ambapo benki itakayoshinda itashindanishwa na mikoa mingine ili kupata mshindi wa kitaifa.

Akifafanua zaidi Dkt Ndugulile amesema kuwa lengo la kuingiza mabenki ni kukumbusha umuhimu wa kuweka miundombinu ya usafi hasa vyoo kwa ajili matumizi ya wateja ambao mara nyingi wamekua wakisahaulika.

Malengo ya Mashindano hayo ni kuongeza ufahamu na uelewa ndani ya jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha Afya na Usafi wa mazingira, kupanua ushirikishwaji wa jamii katika kushughulikia masuala ya Afya na usafi wa mazingira, kuiwezesha jamii kubadili tabia na mazingira wanayoishi kwa kuzingatia usafi na kanuni za afya.

Malengo mengine ni pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika kutoa huduma za usafi wa mazingira na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji na wadau mbalimbali katika suala la usafi wa mazingira.

Mashindano haya yataendeshwa na Kamati ya Taifa ya mashindano ya usafi wa Mazingira inayojumuisha wajumbe kutoka katika Wizara na Taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Wizara ya Elimu Sayansi na Tekonolojia, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.

Post a Comment

0 Comments