habari Mpya


Muleba Yapatiwa Milioni 194 na Japan Kujenga Zahanati ya Mafumbo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Ndg. EMMANUEL SHEREMBI akisaini mkataba huo na Ubalozi wa Japan, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji Halmshauri ya Wilaya Muleba, Ndg. EMMANUEL SHEREMBI  tarehe 15 Machi, 2019 amesaini Mkataba wa Tzs. milioni 194,297,000.00 na Ubalozi wa Japan  baada ya andiko la ujenzi wa zahanati ya Mafumbo lililoandikwa na Halmashauri ya wilaya ya Muleba kukidhi vigezo vya kupewa fedha hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ndg. EMMANUEL SHEREMBI ameshukuru ubalozi wa Japan kwa kukubali kufadhili ujenzi huo na kuahidi fedha hizo zitatumika kama zilivyokusudiwa ili kuwasaidia Wananchi wa kata ya Mafumbo na kata za jirani waliokuwa wanatembea umbali mrefu kupata huduma za afya. 

Aidha, amesema kuwa akina mama na watoto walikuwa wanahangaika kufuata huduma za kliniki umbali mrefu lakini kwa ujenzi wa miundombinu hii, sasa tatizo hili litaisha na wanajamii watapata huduma kwa wakati.

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ni miongoni mwa Halmashauri 7 tu kati ya Halmashauri 185 Tanzania ambazo zimefanikiwa kupata ufadhili huo na  kwa mkoa wa kagera ikiwa ni Halmashauri pekee iliyopata ufadhili huo.

Fedha hizo zitatumika kujenga majengo ya OPD, RCH, Nyumba ya Mganga na vyoo kuanzia hatua ya msingi hadi kukamilika pamoja na ununuzi wa samani. 

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mhe.CHARLES MWIJAGE (MB), Mbunge Jimbo la Muleba Kaskazini. 

Imetolewa na Kitengo cha:
Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

Post a Comment

0 Comments