habari Mpya


Tanzania yatoa Msaada kwa Nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe Baada Kimbunga Idai.

Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa dawa, chakula na vifaa vya kujihifadhi kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa kimbunga cha Idai kilichosababisha mafuriko yaliyozikumba nchi hizo tangu wiki iliyopita.

Msaada huo umekabidhiwa kwa Mabalozi wa nchi hizo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
 
 
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Pro. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakiwa na Mabalozi wa Msumbiji, Malawi  na Balozi Mdogo wa Zimambwe nchini wakipokea misaada ya madawa na vyakula ambavyo serikali ya Tanzania imetoa kwa nchi zao .
Sehemu ya msaada huo utapelekwa nchi za Malawi, Zimbabwe na Msumbiji unatarajiwa kusafirishwa kwa kutumia ndege za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
 
 Askari wa Jeshi la Ulinzi wakishusha misaada ya madawa na chakula ambavyo serikali ya Tanzania imetoa msaada kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe  ambazo zimekumbwa na maafa ya mafuriko. 
Akizungumza wakati zoezi la kupakia msaada huo katika ndege ya Jeshi likiendelea Mhe. Prof. Kabudi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kutolewa kwa msaada huo sambamba na salamu za pole kwa Marais wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe pamoja na wananchi wa nchi hizo kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo.

"Rais Magufuli baada ya kupata taarifa hizi na kuzungumza na Marais wenzake wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, Tanzania imeona ni vyema kutokana na undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze kuwapelekea msaada angalau kidogo wa dawa na chakula na pia kuwapa pole kwa maafa haya makubwa yaliyowapata" amesema Prof. Kabudi. 
Brigedia General Francis Mushi wa kikosi cha anga cha JWTZ akiongea na wanahabari baada ya kukabidhiwa misaada ya madawa na chakula ili kuipeleka nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe  ambazo zimekumbwa na maafa ya mafuriko yaliofanyika mapema mwezi huu yamezidishwa na kimbunga Idai ambacho kilikumba eneo la kaskazini mwa Msumbiji mnamo tarehe 15 mwezi Machi 2019 na kusababisha unahiribifu mkubwa wa nyumba , shule, hospitali na miundo mbinu.

Post a Comment

0 Comments