habari Mpya


Ukatili wa Kingono dhidi ya Watoto Waongezeka-TGNP.

Janeth Mawinza, msemaji na mfuatiliaji wa vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto akizungumza na waandishi wa Habari

Matukio ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto yanadaiwa kuongezeka nchini ambapo inaelezwa kuwa mmoja kati ya wasichana watatu na mmoja kati ya wavulana saba hukutana na hali hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa na Mtandao wa TGNP ambao imesema kati ya watoto watatu wa kike mmoja amekutana na hali ya ukatili wa kingono na kwa upande wa watoto wa kiume saba mmoja wao ameshakutana na ukatili wa kulawitiwa.

Kwa mujibu wa mtandao huo, kufuatia kuongezeka kwa vitendo hivyo, wameamua kuja na kampeni ya ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa kingono.

Aidha wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mtandao huo umesema, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2018, inaonesha watoto 394 kila mwezi walifanyiwa ukatili wa kingono sehemu mbalimbali na kati ya hayo matukio 12 hadi 34 yalifanyika katika kipindi cha Januari hadi Juni 2017 huku kwa kipindi cha Januari  - Juni 2018 yaliripotiwa matukio 533 ikiwa ni ongezeko mara dufu la ulawiti wa watoto.

Kwa mujibu wa  Janeth Mawinza, mfuatiliaji wa matukio na mmoja wa wadau wa kupinga matukio ya ukatili wa kingono amesema lengo la kujitokeza kuendesha kampeni hiyo ni kwa ajili ya kutatua ulinzi na changamoto ya mtoto dhidi ya ukatili wa kingono.

Mwanaharakati huyo amesema, ukatili dhidi ya watoto umekuwa ni sehemu ya maisha ya watoto hao na kwamba wapo baadhi wamefanikiwa kuripoti dhidi ya vitendo hivyo na kupatiwa msaada huku wengine taarifa zao zikiwa ni siri na hivyo kukosa msaada.

Amesema taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu imeutaja Mkoa wa Dar es Salaam  kuongoza kwa vitendo hivi huku wengi wa wanaofanyia watoto hao wakidaiwa kuwa ni waathirika wa vitendo hivyo wanaodaiwa kulipa kisasi.

Wanaharakati hao wamekuja na Kauli Mbiu, Tanzania bila ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto inawezekana Jamii iguswe na ichukue hatua ya kumlinda mtoto popote alipo nje na ndani ya shule.

Source-Azam tv

Post a Comment

0 Comments