habari Mpya


Taswira Picha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwasili Mkoani Kagera Kwa Ziara ya Siku mbili.

Na: Sylvester Raphael

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa  akiwasili Mkoani Kagera tarehe 20 Februari, 2019 kwa ziara ya siku mbili  ambapo mara baada ya kuwasili Nyakanazi Wilayani Biharamulo akitokea Mkoani Kigoma akipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti sambamba na Viongozi mbalimbali wa Kiserikali ,Chama na Wananchi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  aliongea na wananchi wa Nyakanazi katika Mkutano wa hadhara na kuwaeleza wananchi jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika Mkoa wa Kagera.
 
Katika Mkutano wa hadhara Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa wito kwa Sekta binafsi pale zinapoaminiwa na Serikali na kupewa miradi ya kutekeleza kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa na kukamilika kwa wakati.

 Waziri Mkuu alisikitishwa na Mkandarasi anayeendelea kujenga barabara ya Nyakanazi Kibondo Kilometa 50 (Nyanza Roadworks Ltd) kutomaliza barabara hiyo kwa wakati pamoja na  kuwa Serikali tayari imeilipa Kampuni hiyo ya Kitanzania fedha za kujenga barabara hiyo.

Sijaridhishwa na kiwango cha ujenzi wa barabara ya Nyakanazi Kigoma, jana nimeongea na Mkandarasi anasingizia hana malori na hana vifaa wakati tayari tumemlipa fedha. Serikali imekuwa ikakaa na Sekta binafsi na kuongea nao na kilio chao kilikuwa ni kuaminiwa na kupewa kazi na Serikali lakini walio wengi hawatekelezi miradi hiyo na kuimaliza kwa wakati mfano hii barabara imeanza tangu mwaka 2014 mpaka sasa bado Mkandarasi anajikongoja tu.” Alieleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa kama Mkandarasi huyo atashindwa kukamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Aprili 2019 Serikali itamfukuza kazi. 

Barabara ya Nyakanazi Kibondo kilometa 50 ilianza kujengwa mwaka 2014 na kulingana na Mkataba ilitakiwa kuwa imekamilika ifikapo Juni 2016 lakini mpaka sasa bado haijakamilika.  Aidha gharama za ujenzi wa barabara hiyo ni bilioni 45.986 mpaka kukamilika hadi kiwango cha rami.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia aliwaeleza wananchi wa Nyakanazi waliokusanyika kumsikiliza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha inakamilisha kwa asilimia 90% miradi yote ya maendeleo ambayo ilihaidiwa wakati wa uchaguzi mwaka 2015 katika sekta za Elimu, Maji, Afya na Miundombinu ya barabara na umeme kwa wananchi ifikapo mwaka 2020.

Mwisho Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa Halmashauri ya Biharamulo kuhakikisha wanasimamia na kukusanya mapato ya Serikali ipasavyo. Pia aliwakumbusha wananchi wa Nyakanazi kuhakikisha wanakuwa wazalendo kwa kutumia mfumo wa nyumba kumi za usalama kuimarisha ulinzi na usalama hasa kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ambao wamekuwa wakija nchini na kufanya vitendo vya uharifu.  

Post a Comment

0 Comments