habari Mpya


RC Gaguti- Mwananchi Atakayejichukulia Sheria Mkononi Kukiona cha Moto.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama KuU Tanzania Kanda ya Bukoba wakati wa kuadhimisha kilele cha wiki ya Sheria Februari 6, 2019 mjini Bukoba.


Akitoa salamu za Serikali katika hafla hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Kagera ameipongeza Mahakama kwa kudumisha utamaduni wa kuadhimisha Wiki ya Sheria tena kwa kutoa msaada wa kisheria na elimu kwa wananchi na baadhi ya makundi mbalimbali ili yaweze kuelewa vizuri namna ya kutafuta haki Mahakamani.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama kupitia vyombo mbalimbali ambavyo vipo chini ya Serikali kukomesha Wanasheria na Mawakili Vishoka wanaowarubuni wananchi na kufanya kazi za kisheria bila weledi wa kutosha na kuwafanya wananchi kuendelea kupoteza muda mwingi Mahakani bila sababu.
Aidha Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa onyo kwa wananchi wanaojichukulia sheria mikononi katika Mkoa wa Kagera kuacha tabia hiyo kwani vitendo hivyo vinaupa mkoa sifa mbaya kama ilivyokuwa katika ujambazi wa kutumia siraha. Alisisitiza kuwa hapo nyuma Mkoa wa Kagera ulisifika kwa matendo ya ujambazi lakini Serikali ilikomesha vitendo hivyo na sasa Kagera ipo katika mikoa inayofanya vibaya katika kujichukulia sheria mikononi.


Akihitimisha Salamu za Serikali Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaomba Viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, uvumilivu na upendo kwa waamini wa madhehebu yote ili wananchi waache vitendo viovu na kumrudia Mwenyezi Mungu jambo ambalo litapunguza kesi Mahakamani na kuwafanya wananchi kutumia muda mwingi kuzalisha na kufanya kazi za kujiingizia kipato. 
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi Lameck M. Mlacha alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati akitolea mfano wa upelelezi wa kesi ya mauaji ya Mwanafunzi Marehemu Spelius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta aliyefikwa na Mauti baada ya kupigwa na Mwalimu Respikius Patrick Mtazangira kufanyika kwa weledi na kwa wakati jambo ambalo lilipelekea kesi kufikishwa mahakani kwa wakati.

Jaji Mfawidhi Mlacha alitoa onyo kwa baadhi ya Mahakimu, Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi, na baadhi ya Makarani katika Mahakama ambao bado wanajihusisha na kupokea au kushawishi kupewa rushwa kuwa wakigundulika watachukuliwa hatua kali kwani zama hizi si zile walizozizoea vinginevyo wabadili mienendo ya tabia hizo mara moja na kutenda haki kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments