habari Mpya


Mfumo Dume Kikwazo kwa Wanawake wilayani Ngara Kutoa Maamuzi Ngazi ya Familia.

Na Aurelia Gabriel –RK Ngara 97.9

Imeelezwa kwamba wanawake walio wengi wilayani Ngara mkoani Kagera, bado hawana nafasi ya kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi kwenye uongozi na hivyo kuzidi kudidimizwa kimaendeleo.

Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Ngara Bi.JOSEPHINA LUSATILA ameiambia redio Kwizera kwamba hali hiyo inasababishwa na mfumo dume ambao bado upo kwa wanaume wa kumuona mwanamke kama mtu asiyeweza.

Hata hivyo amewaasa wanaume kubadili fikra hizo kwani wanawake ambao wamekuwa wakipewa nafasi za uongozi wameonekana kufanya vizuri zaidi hata ya wanaume.

Nao baadhi ya wanawake wilayani Ngara waliozungumza na Redio Kwizera wamesema wanaume wasiwe na mitazamo hasi juu ya usawa wa kijinsia bali washirikiane katika kufikia maendeleo.

Baadhi ya wanawake pamoja na wadau wa maendeleo wilayani Ngara leo wamekutana katika ukumbi wa halmashauri kujadiliana namna ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika Machi 8 ya kila mwaka na kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘BADILI FIKRA KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA KWA MAENDELEO ENDELEVU’

Post a Comment

0 Comments