habari Mpya


Hadi Februari 1, 2019 Vitambulisho 16,369 Vyenye Shilingi Milioni 327 Vyagawiwa Kagera.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali MARCO E. GAGUTI amegawa vitambulisho 35,000 vya awamu ya pili vya Wafanyabiashara Wadogo katika Mkoa wa Kagera na kuwaagiza Watendaji wa Serikali chini ya usimsmizi wa Wakuu wa Wilaya kuendelea na zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo na kuhakikisha ifikapo Februari 28, 2019 vitambulisho vyote view vimegawiwa kwa Wafanyabiashara Wadogo.

Katika hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho hivyo 35,000 vya awamu ya pili kwa Wakuu wa Wilaya iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Februari 1, 2019 Mkuu wa Mkoa GAGUTI alisema kuwa katika tahimini iliyowakutanisha Wakuu wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara Mkoa wa Kagera haukufanya vizuri sana wa vibaya katika ugawaji wa vitambulisho vya awamu ya kwanza 25,000 kwani ulishika nafasi ya sita kwa ugawaji wa asilimia 65%.
Mkuu wa Mkoa GAGUTI katika hafla hiyo fupi aliziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinakusanya takwimu za Wafanyabiashara wote Wakubwa, wa Kati na wale Wadogo ifikapo Februari 15, 2019 takwimu hizo ziwe zimewasilishwa ofisini kwake lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anayetoa bidhaa yoyote na kupokea fedha anatambuliwa na kulipa kodi au tozo stahiki za Serikali.

Hafla hiyo fupi iliyowashirikisha Wakuu wa Wilaya saba za Mkoa wa Kagera, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa, Wenyeviti wa Halmashauri na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba, Watendaji wa Kata wa Manispaa ya Bukoba waliowawakilisha Watendaji wenzao katika mkoa ambao walitakiwa kutoa changamoto zinazowakumba katika ugawaji wa vitambulisho vya Wafanyabiashara Wadogo katika maeneno yao.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Wakitoa changamoto mbalimbali  kuhusu ugawaji wa vitambulisho Watendaji wa Kata walisema kuwa changamoto kubwa ni Elimu kwa wananchi kutojua ni mfanyabiashara yupi anatakiwa kupata kitambulisho na ni yupi hastahili kupata na changamoto hiyo inatokana na suala la mauzo ghafi kutoeleweka vizuri kwao wao wenyewe Watendaji  kama wahusuika wa ugawaji lakini pia wafanyabiashara jambo ambalo waliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa uelewa kwao.

Changamoto nyingine iliyotajwa na Watendaji wa Kata waliohudhuria hafla fupi ya kukabidhi  vitambulisho kwa Wakuu wa Wilaya  ni suala la Mfanyabiashara Mdogo kuwa na namba ya utambuzi ya mlipa kodi ya TRA (TIN) wakati biashara yake ni ndogo na hastahili kupata kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo wakati mtaji wake ni mdogo haufikii kiwango cha shilingi milioni 4,000,000/= kwa mwaka.

Akitoa majibu ya  changamoto zilizowasilishwa na Watendaji wa Kata Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Kagera Bw. ADAM NTOGA alisema kuwa Mfanyabiashara Mdogo anayestahili kupata kitambulisho ni yule ambaye mauzo yake kwa siku hayafikii shilingi 11,000/= kwa siku. Kama Mfanyabiashara anauza bidhaa zake na kupata kiwango cha fedha chini ya shilingi 11,000/= huyo anastahili kupata kitambulisho cha Mfanyabiashara Mdogo.

Hata kama Mfanyabiashara ana mtaji wa shilingi 5,000/= lakini anauza bidhaa zake kwa siku na kupata shilingi 11,000/= au zaidi kwa siku huyo hastahili kupata kitambulisho, kinachoangaliwa hapa si mtaji wa mfanyabiashara alionao bali ni mauzo yake kila siku kama anapata kiasi cha shilingi 11,000/= au chini ya kiwango hicho.” Alifafanua Bw. Adamu Ntoga 

Katika huatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa onyo kwa Wafanyabiashara ambao walidanganya na kupokea vitambulisho wakiwa tayari wametambuliwa na mfumo wa ulipaji kodi wa TRA kuwa tayari anayo amajina sita hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwao mara moja. 

Pia aliwaonya Watendaji wa Kata ambao wanaandika barua kuwatambulisha wafanyabiashara kuwa mtaji wao ni mdogo kuwa waache mara moja.

“Watendaji wa Kata acheni hizo tabia zenu za kuwaandikia barua wafanyabiashara na kuwatambulisha kuwa biashara zao ni ndogo, kama kuna Mfanyabiashara alipita TRA na kujisajiliwa mwacheni apite huko huko na kufanyiwa tathimini upya na TRA wao ndiyo watoe barua hizo vinginevyo mkiendelea hatua zitachukuliwa kwenu.” Alionya Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Aidha, Mkuu wa Mkoa alitoa ufafanuzi juu ya Wafanyabiashara Wadogo wanaopata vitambulisho kuendelea kutoa tozo ndogo ndogo za Halmashauri husika katika maeneo wanayofanyia biashara mfano tozo za kukusanya taka au huduma za vyoo na usafi na kuwataka kutotumia kigezo cha vitambulisho na kuacha kulipa tozo hizo. 

Pia Wafanyabiashara ambao tayari wanatakiwa kulipa kodi katika Halmashauri wanatakiwa kuendelea kulipa kodi hizo baada ya kufanyiwa tathimini na TRA. 

Mkoa wa Kagera katika awamu ya kwanza ulipatiwa vitambulisho vya Wafanyabiashara Wadogo 25,000 na Wilaya ya Bukoba ilipatiwa jumla ya vitambulisho 3,580. Wilaya za Missenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Muleba, na Biharamulo zilipatiwa vitambulisho 3,570 kila moja. 

Hadi tarehe 1 Februari,2019 vilikuwa vimegawiwa vitambulisho 16,369  sawa na asilimia 65% kwa Wilaya zote na kiasi cha shilingi milioni 327,380,000/= zilikuwa zimekusanywa na kupelekwa benki.

Vitambulisho vya awamu ya pili Mkoa wa Kagera ulipatiwa vitambulisho 35,000 na vitambulisho hivyo vimegawiwa katika Wilaya kulingana na Jiografia ya Wilaya, wingi wa watu na hali ya kiuchumi tofauti na awamu ya kwanza ambapo katika awamu ya pili Wilaya Bukoba iligawiwa vitambulisho 7,000 Biharamulo na Ngara kila moja iligawiwa vitambulisho 4,200.
 
 Kyerwa na Missenyi kila moja vitambulisho 4,400 na Wilaya za Karagwe na Muleba ziligawiwa vitambulisho 5,400.

Post a Comment

0 Comments