habari Mpya


Ukosefu wa Maadili Kiutendaji na Utawala Bora Changamoto ya Amani ya Kudumu Afrika.

 JOSEPH ODUOR AFULO.

 Na Shaaban Ndyamukama –RK Ngara 97.9

Ukosefu wa maadili mema kiutendaji,  misingi ya utawala bora na utii wa sheria  kutoka kwa Viongozi waliopewa mamlaka kwenye mataifa mbalimbali ni baadhi ya vikwazo vinavyohatarisha haki za binadamu na kukosekana amani ya kudumu Barani Afrika.

Mkuu wa Shirika la Mapadre (Jesuit Fathers) Afrika mashariki JOSEPH ODUOR AFULO amebainisha hayo  January 21.2019  baada ya kutembelea wilaya ya Ngara mkoani Kagera kuhamasisha Mapadre waliojiunga na Shirika hilo  kulinda amani na utulivu wanakopangwa kufanya kazi za kiroho. 

Shirika la Mapadre ukanda wa Afrika Mashariki unajumuisha nchi ya Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia , Sudani Kusini na Kaskazini ambapo  Mapadre wa Shirika hilo husimamia miradi ya Elimu, Afya , Huduma kwa Wakimbizi (Jesuit Refugees Service) Amani na Maridhiano na  Kulinda haki za Binadamu   Barani Afrika.

Padre AFULO amesema Bara la Afrika limepoteza amani na utulivu kutokana na Viongozi wenye dhamana kutofuata misingi ya utawala bora,  kukuza demokrasia lakini pia baadhi yao hawatumii kanuni na sheria kulinda maslahi ya  mataifa  wanayoyaongoza baada ya kupatiwa dhamana na wananchi au mamalaka zinazohusika.

"Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, wanaokiuka haki za binadamu wanakosa malezi  kifamilia, kutokuwa na adabu na utii vilevile kukiuka misingi ya kiroho katika makanisa na misikiti licha ya kuonekana watu wema mchana lakini usiku wanafanya kinyume" Amesema AFULO

Alisema mataifa mengi yamekosa mwelekeo wa amani na utulivu yemejaa  mateso, kuwepo changamoto ya vurugu za kisiasa, kiuchumi na kijamii lakini pia utendaji wa viongozi wa kisiasa umekuwa wa kujichukulia maamuzi badala ya kufuata waliyotumwa na waliowachagua.

Amesema watu duniani na mamlaka husika kuwepo ukweli katika kutamka na kutenda kudumisha amani badala ya kusababisha machafuko, vita na dhuluma na kila mmoja aguswe na tatizo la mwingine kwa kuanzia ngazi ya familia ili kuwepo usalama kila taifa.

Amesema pia mifumo ya elimu inayotolewa hivi sasa kwa kuhamasishwa na viongozi wa serikali mataifa mbalimbali duniani haiwajengi wananchi kujitegemea na kusababisha matabaka kwani watoto wa viongozi husomea katika shule zenye gharama kubwa huku wakiwa tegemezi kiakili.

Akizungumza kwa kutumia  lahaja na methali za Kiswahili, amesema  kabla ya uhuru  wanafunzi walijifunza elimu ya kujitegemea ,kwa sasa wanalundikiwa masomo mengi  wakijifunza kujibu mitihani kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu na kila anayepata  nafasi anakuwa fisadi kwa kila mbinu ili kujinufaisha.

"Inafaa wazazi kuwalea watoto kwa nidhamu maana  Aja ya mja hunena  lakini kutolewe  elimu ya kujitegemea kuepuka kupata viongozi na watendaji mafisadi ,wala rushwa na wenye kukiuka haki za wengine" Aliongeza.

Akiwa wilayani Ngara aliwapongeza wandishi wa habari wa Radio Kwizera   kwa utendaji kazi  wao katika kuhabarisha jamii na kuhimiza utawala bora, upatikanaji wa haki za binadamu na kwamba  lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kutaka kujua hali ya  majesuit kwa  huduma wanazofanya hatimaye kubaini changamoto zilizopo   na jinsi ya kuzitatua.

Awali akiwa na wenyeji wake wilayani Ngara Padri FREDRICK MEELA amesema katika kusimamia majukumu na utendaji wa shirika hilo  kwa wilaya  ya Ngara na wilaya zinazounda mkoa wa Kigoma wananchi wanapata huduma za kuwajenga kiroho na kuwapa matumaini ya Amani

Amesema upashanaji wa habari hupitia njia ya Radio Kwizera  kwa kuweka wanahabari maeneo mbalimbali zikiwemom kambi za wakimbizi mkoani Kigoma lakini hata maeneo mengine  kwa baadhi ya  mikoa ya  kanda ya ziwa Viktoria  lengo kuhamasisha jamii kujiletea maendeleo

“ Mpango wetu ni kupanua matangazo baada ya radio yetu   kuelimisha  jamii na kuaminiwa ikiwa ni  ya saba kitaifa  kati ya  Radio 168 zenye usajili nchini Tanzania  ikitumika kuimarisha umoja na amani na  misingi ya utawala bora” Alisema padre Meela

Amesema  pia mapadre hao wanasimamia elimu  maeneo mbalimbali nchini kama  vile Loyola iliyoko Mabibo jijini Dar es Salaam, St Peter Claver ya mkoani Dodoma  zikiwemo shule za msingi  lakini pia  shule hizo hutoa huduma za afya kwa ajili ya wanafunzi na walimu.

Post a Comment

0 Comments