habari Mpya


Majengo ya Mradi wa ( Izigo AP) Muleba Yakabidhiwa na Shirika la World Vision Tanzania.

Shirika la World Vision Tanzania limekabidhi majengo yaliyojengwa na mradi wa World Vision(Izigo AP) kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji Kabuleme, Kata Izigo, Wilaya ya Muleba,mkoani Kagera.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shule ya Msingi Kabuleme, Meneja Kanda ya Kagera Bi. JULIANA CHARLES ameeleza kuwa mnamo mwaka 2017 mradi wa maendeleo Izigo ulipokea barua kutoka shule ya msingi Kabuleme iliyoainisha matatizo makubwa yanayoikumba shule hiyo, likiwemo tatizo kubwa la uhaba wa madarasa, choo cha wanafunzi na walimu pamoja na madawati. 


Baada ya mradi kupokea taarifa hiyo walifika shuleni hapo na kuona hali halisi ya mazingira ya shule na ufundishaji kwa ujumla. 

Ndipo walipoandikia andiko na kupitia wafadhiliwa wa nchi ya Ujerumani, andiko liliweza kupata Tzs. 76,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, matundu 5 ya vyoo vya wanafunzi, tanki la maji ya kunawa mikono lenye ujazo wa lita elfu tano, madawati 60 na mipira 6 ya michezo.
Akipokea majengo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Ndg. EMMANUEL SHEREMBI ameendelea kushukuru sana shirika la World Vision Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa wilayani Muleba ikiwemo ujenzi na ukarabati wa zahanati ya Bushekya, ujenzi wa zahanati Bugasha, ujenzi wa miundombinu shule ya msingi Kabuleme na ujenzi wa jengo la mama na mtoto kituo cha afya Izigo."Msichoke kutufadhili katika sekta za Elimu na Afya kwani Wilaya ya Muleba ina uhaba mkubwa sana wa miundombinu ya Elimu na Afya hali inayopelekea jamii kukosa huduma hizo za muhimu. Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha miundombinu hiyo lakini bado uhitaji ni mkubwa", ameeleza Ndg. EMMANUEL SHEREMBI.
Majengo yaliyokabidhiwa ni pamoja na vyumba vitatu vya madarasa vyenye thamani ya Tzs. 60,132,210.00 ambapo Shirika la World Vision limechangia Tzs. 54,512,210.00 na jamii imechangia Tzs. 5,620,000.00, ujenzi wa matundu matano ya vyoo na ununuzi wa tanki la maji wenye thamani ya Tzs. 14,693,360.00, ununuzi wa madawati 60 kwa jumla ya Tzs. 5,160,000.00 na ununuzi wa mipira 6 ya michezo yenye thamani ya Tzs. 435,000.00. Jumla ya gharama za ujenzi na vifaa ni Tzs.80,420,560.00.Imetolewa na:

Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Mahusiano,

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

Post a Comment

0 Comments