![]() |
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kusitishwa
mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika
maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana
ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji
hivyo.
Rais
Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 15
Januari, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangallah,
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John
Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph
Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bi. Dorothy Mwanyika.
|
![]() |
“Mimi sifurahii kuona wafugaji kila mahali wanafukuzwa, kama
kuna eneo ambalo tunafikiri lilikuwa hifadhi ya wanyama lakini halitumiki,
tutabadilisha sheria, tunalimega na tunaligawa kwa wafugaji, vivyo hivyo hata
kwa wakulima kama kuna eneo tunaona ni hifadhi lakini halina msitu wala
wanyamapori, na lina rutuba, na wakulima wanataka kulima nalo tunalimega
tunawapa wakulima.
Baadaye tutajua kabisa eneo hili ni la hifadhi,
hili ni la mifugo, hili ni la wakulima, hili ni la makazi. Kwa hiyo nyinyi
Mawaziri na Makatibu Wakuu mkakae mkatangulize maslahi ya hawa tunaowaongoza
ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi nakadhalika, lakini pia tunahitaji
wanyamapori, sijasema sasa hifadhi zote za wanyama tunazimaliza, hapana,
hifadhi za wanyama lazima tuzihifadhi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameagiza vijiji vyote 366
vilivyoainishwa kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi hapa nchini visiondolewe
katika maeneo hayo na badala yake ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa wizara
zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji hivyo na kuanzisha mchakato wa
mabadiliko ya sheria ili yawasilishwe katika kikao kijacho cha Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
|
![]() |
Amefafanua
kuwa ni lazima Serikali ifanye maamuzi haya sasa kwa kuwa idadi ya Watanzania
imeongezeka hadi kufikia Milioni 55, idadi ya mifugo imeongeza hadi kufikia
Milioni 35 na hivyo kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya maeneo ya ardhi
ikilinganishwa na wakati nchi inapata uhuru ambapo Watanzania walikuwa Milioni
9 na mifugo ilikuwa Milioni 10.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza sheria ya vyanzo vya
maji pia iangaliwe upya ili kutowazuia Watanzania wanaozalisha mazao kandokando
mwa mito na ameelezea kutofurahishwa kwake na vitendo vya kufyeka mazao ya
wakulima kwa madai kuwa wamelima ndani ya mita 60.
Halikadhalika
Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasilisha kwake mapendekezo ya
kufutwa kwa mashamba ambayo hayajaendelezwa na ameagiza wizara hiyo iendelee
kumpelekea mapendekezo ya mashamba yote yaliyotelekezwa ili ayafute na wananchi
wagawiwe kwa ajili ya kuyatumia kwa uzalishaji wa mazao na mifugo.
Hata hivyo Rais
Magufuli amesema maagizo hayo hayana
maana kuwa sasa wananchi waruhusiwe kuvamia maeneo ya hifadhi, na ametaka zoezi
la uwekaji wa mipaka lifanyike haraka na kwa uwazi.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari,
2019.
|
0 Comments