habari Mpya


Serikali Yawataka Watanzania kujitokeza Kupima VVU kwa Hiari.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha Kitabu cha mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti maambukizi ya VVU nchini Tanzania.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kujitokeza kupima afya zao  kwa hiari huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za Upimaji wa Virusi vya UKIMWI  ili kuzuia maambukizi  mapya ya Virusi Vya Ukimwi.

 Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo jijini Dodoma wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambapo pia amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wenye lengo la kupunguza Maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 hadi 2023.

Majaliwa akihutubia wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo amesema katika utekelezaji wa mkakati huo, ni lazima kuimarisha mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau pamoja na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa  katika mkakati huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, Dkt. Lenard  Maboko amesema mwamuko wa wanaume kujitokeza kupima VVU kwa sasa umeanza kuimarika zaidi.

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani hufanyika Disemba Mosi kila mwaka ambapo kwa  mwaka huu yamefanyika jijini Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, “PIMA, JITAMBUE, ISHI”.

Katika maadhimisho hayo Waziri wa Ofisi ya Waziri mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama na Naibu Waziri wa Afya, walikuwa ni miongoni mwa viongozi walioshuhudia uzinduzi wa mkakati huo wa nne wa Taifa.

Katika hatua nyingine, Mkoa wa Njombe  ambao umeongoza kwa kuwa na   kiwango kikubwa  cha maambukizi cha asilimia 11.6 ambacho ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.7  umeanza kuonesha mafanikio kwa jamii juu ya kupima na kutambua hali zao.

Hatua hiyo imedaiwa kuja kufuatia kuongeza jitihada za utolewaji  wa elimu ya kujitambua inayokwenda sambamba na uhamasishaji katika upimaji na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza virusi.

Wakati huo huo , Licha ya Zanzibar kufanikiwa kuwa na kiwango kidogo cha watu wanaoishi na VVU ambao ni asilimia 0.4 bado suala la unyanyapaa wa jamii na unyanyapaa binafsi kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, limeendelea kutatiza juhudi za mapambano ya maambukizi ya mapya ya Virusi vya Ukimwi katika maeneo mengi nchini.

Hadi sasa jumla ya watu 6,393 wanadhaniwa kuishi na Virusi Vya Ukimwi visiwani Zanzibar wengi wao wakiwa ni kati ya miaka 30 hadi 49.

Post a Comment

0 Comments