habari Mpya


Operesheni Sangara 2018 Kagera yakamata Zana Haramu za Uvuvi Elfu 21.

Bw.Didas Mtambalike.

 Na Shaaban Ndyamukama RK Muleba 97.7

Zoezi la kuwasaka wavuvi  haramu na wafanya biashara wa samaki linaendelea chini ya kauli mbiu ya Operesheni Sangara 2018 likisimamiwa na maafisa wafawidhi  usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya ziwa Viktoria.

  Afisa mfawidhi wa usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi mkoa wa Kagera Westi Mbembati amesema katika zoezi la ukamataji samaki wanaouzwa au kuvuliwa kinyume cha sheria, zaidi ya kilo 1,740 wamekamatwa huku nyavu za kuunganishwa kwa kutengenezwa kienyeji ni 9,000.
Mbembati ametoa taarifa hiyo akihutubia wakazi wa kijiji cha Ihumbo kata ya Bumbile ambapo doria inawasaka na kuwakamata wavuvi walioko katika kisiwa hicho  na kisiwa cha Rubiri kilichopo kata ya Mazinga wilayani Muleba.

Amesema pia zimekamatwa  ndoano zinazovua samaki wakubwa 11,237 na kwamba  wafanya biashara wengi wanasafirisha samaki kwa kuwachanganya halali na haramu ingawa wanaonyesha leseni na vibali halali.

Pia amesema wafanyabiashara wanapaswa kuwa na vielelezo bila kutoa rushwa  barabarani kama kuonesha Leseni ya biashara, Leseni ya kusafirisha samaki, Leseni ya ukusanyaji rasirimali za uvuvi na kibali cha usafirishaji.

 Aidha amesema imekamatwa mitumbwi 28 yenye kufungiwa injini inayotumika katika uvuvi haramu ,kamba za makokolo 405, nyavu za timba 403, nyavu za dagaa  48 huku ukifanyika ukaguzi wa mitumbwi na boti 200  iliyosajiliwa. 
 
Naye Afisa mfawidhi Usimamizi na Ulinzi wa Rasirimali za Uvuvi kanda ya ziwa Didas Mtambalike amewataka wavuvi kuunda umoja wao na kujiunga katikavikundi kuanzisha ushirika wa wavuvi kwa kupata mikopo serikalini.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wameipongeza serikali kudhibiti uvuvi haramu kwa kuongeza samaki viwandani na ajira kwa vijana lakini wakaiomba kudhibiti viwanda vinavyozalisha nyavu za samaki na dagaa zisizohitajika. 

Post a Comment

0 Comments