habari Mpya


Namna Mkakati wa Nyumba Kumi Bora za Usalama Utakavyofanya Kazi-Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti amezindua rasmi mkakati wa kuimarisha USALAMA katika Mkoa wa Kagera ukiwa na lengo la kukomesha UHALIFU, UJAMBAZI NA VITENDO VYA UVUNJIFU WA AMANI katika Mkoa wa Kagera alizindua Mkakati huo kimkoa wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” wenye kaulimbiu isemayo: 10 BORA! Usalama wa Nchi, katika Kijiji cha Chabuhola, Kata Nyakabanga Tarafa Nyakakika Wilayani Karagwe Novemba 1, 2018.
Namna Mkakati wa Nyumba Kumi Bora za Usalama Utakavyofanya Kazi.

Kila Kijiji zinatengwa nyumba kumi kumi na kila nyumba kumi anachaguliwa kiongozi mmoja ambaye anajua kusoma na kuadika. Kila nyumba au kaya wanaorodheshwa wanafamilia wanaoishi katika nyumba hiyo na kunakuwa na orodha ya kila nyumba kwa nyumba zote kumi.

Majukumu ya Kiongozi ni kuhakikisha katika nyumba zake kumi hakuna mgeni anayeingia au kuishi bila kuwa na taarifa za mtu huyo ametokea wapi au amekuja kufanya nini katika eneo hilo. Jukumu la mwananchi ni kutoa taarifa kwa Kiongozi wa Nyumba Kumi za Kiusalama apatapo wageni na taarifa za muhimu za mgeni huyo ili kuzuia uvunjaji wa amani kwa watu wasiojulikana wanatokea wapi au wamekuja kufanya nini.

Aidha, katika kuzuia wizi wa mifugo wananchi watatakiwa kutoa taarifa kwa Kiongozi wao pale wanapotaka kuchinja mbuzi au ngombe kwaajili ya kuuza au kitoweo cha nyumbani katika familia zao ili Kiongozi ahahkikishe kuwa mnyama huyo si wa wizi.

Viongozi wa Nyumba Kumi za Kiusalama wanapewa mihuli iliyo na namba ziatakazotofautisha Vijiji na Kata ambapo wataruhusiwa kuandika barua za kuwatambua wakazi wao na kuwatolea taarifa mbalimbali kwa viongozi wao wa juu. Wasimamizi wakuu wa viongozi wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama ni Watendaji wa Vijiji pamoja na Watendaji wa Kata.

Kila Nyumba Kumi za KIusalama wananchi na kiongozi wao watatakiwa kufanya mikutano ya kujadili ulinzi na usalama kila mwezi na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwa mtendaji wa Kijiji ambapo naye ataunganisha taarifa hizo na kuziwasilisha kwa Afisa Mtendaji wa Kata. Taarifa hizo zitaenda mpaka ngazi ya Wilaya hadi Mkoa ili kama kuna changamoto kubwa ya kiusalama ifanyiwe kazi kwa wakati.
Katika hafla hiyo fupi ya uzinduzi wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama zilitolewa mada kuhusu Urai kutoka Ofisi ya Kamanda wa Uhamiaji Mkoa, Usalama wa Raia kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera . 

Aidha, uzinduzi huo ulihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera. Kuwa kiongozi wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama si ajira ya kulipwa mshahara wala posho bali ni uzalendo wa mwananchi mwenyewe kushiriki katika kulinda usalama wa nchi.
Nao wananchi wa Kata ya Nyakabanga walifurahi na kupokea mkakati huo kwa mikono miwili ambapo walisema kuwa sasa huo unakwenda kuwa mwarobaini wa kukomesha uhalifu, mauaji na magendo. “Wahamiaji haramu wanakuja hapa wanafanya matendo maovu kama mauaji alafu tunaonekana ni sisi wakazi wa hapa kumbe siyo sasa huu mpango wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama utatusaidia sana katika kuwatambua haraka na tunamshukuru Mkuu wa Mkoa.” Alieleza Bw. Amosi Balikweba.

Post a Comment

0 Comments