habari Mpya


Mkoa wa Kagera Katika Uchumi wa Viwanda Tofauti na Viwanda Vya Kusindika Kahawa.


Pamoja na  Mkoa wa Kagera kuwa umejikita katika uchumi mkubwa wa viwanda vya Kahawa lakini pia Mkoa huo unafanya maajabu katika Nyanja ya viwanda vingine kikiwemo kiwanda cha kuchenjua madini ya bati kinachojulikana kwa jina la TANZAPLUS kilichopo Wilayani Kyerwa.

 Kiwanda cha TANZAPLUS kilichopo Kijiji cha Kagenyi Kata ya Kyerwa Wilayani Kyerwa kimeleta mapinduzi makubwa ya uzalishaji wa madini ya bati hasa kwa kuongeza samani ya madini hayo yanayochimbwa katika Kata ya Kyerwa na kuuuzwa kwa bei stahiki lakini kuongeza ajira kwa wachimabaji wadogo kwa kuwa madini hayo sasa yana soko linaloaminika hapo hapo Wilayani Kyerwa.

Sasa mkoa wa Kagera nao hauko nyuma katika Uchumi wa Viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano , Mkoa wa Kagera haujabaki nyuma unatekeleza kikamilifu Sera hiyo kwa kuanzisha, kujenga na kundesha viwanda vya aina mbalimbali lakini pia kuendelea na juhudi za kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali kuja Kagera kuwekeza katika viwanda vya aina mbalimbali.

Kwa miaka mingi madini ya bati yanayochimbwa Wilayani Kyerwa yalikuwa yakitoroshwa na kuuzwa katika nchi jiarani ya Rwanda tena kwa bei ndogo sana jambo ambalo lilikuwa likiinufaisha nchi hiyo wakati madini yanachimbwa hapa nchini katika Mkoa wetu wa Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Rashid Mwaimu akitembelea kiwanda hicho kuonesha jinsi Wilaya ya Kyerwa inavyotekeleza Sera ya Tanzania ya Viwanda alisema kuwa TANZAPLUS imekuwa mkombozi sana kwa vijana ambao ni wachimbaji wadogo kujihusisha zaidi na uchimbaji wa madini ya bati kwani sasa wamepata soko ambapo wanauza madini yao wakiwa ndani ya nchi na madini hayo yanachenjuliwa Wilayani hapo kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi yakiwa tayari yameongezwa thamani.

Tumekuwa tukinyonywa sana hasa katika Wilaya yetu ya Kyerwa madini haya ya bati yanachimbwa hapa lakini yalikuwa yakiuzwa nje ya nchi tena hapa kwetu walikuwa wananunua kilo moja shilingi 15,000/= hadi 18,000/= tu lakini madini hayo hayo yakivushwa tu mpaka na kupelekwa nchini Rwanda yanauzwa hadi shilingi 48,000/= kwa kilo moja unaweza kuona unyonyaji ulivyo tene bila kulipa kodi ya Serikali.” Alieleza Mkuu wa Wilaya Rashid Mwaimu.

Mwekezaji Mzalendo ambaye ni Mtanzania Bw. Salim Mhando amabye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha TANZAPLUS alisema kuwa pamoja na kuchenjua madini ya bati lakini kiwandani hapo lakini wameanza kutengeneza nyaya ambazo zinatumika katika matengenezo ya Kompyuta, Mashine za X ray, kutengeneza vipuli vya Tansfoma za kufua umeme, pia kutengenzea nyaya za kuyeyuesha katika uchomeleaji wa vifaa vya "elektroniki" (zijulikanazo kama risasi)
Kuwepo kwa kiwanda cha TANZAPLUS Wilayani Kyerwa kutaongeza ajira kwa vijana lakini pia kubadilisha mtazamo wa wananchi wa Wilaya hiyo katika kunufaika na madini yanayochimbwa katika Wilaya yao pia Mkoa wa Kagera nao unakua kiuchumi kwa kuongeza ajira kwa vijana na kuzalisha bidhaa kutoka Kagera.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akizungumzia Sera ya Tanzania ya Viwanda na Kagera ya Viwanda anasema kuwa Mkoa wa Kagera umepiga hatua kubwa katika viwanda ambapo hadi kufikia Mwezi Oktoba 2018 Mkoa ulikuwa na viwanda 502 ambapo kati hivyo viwanda vikubwa ni tisa (9), vya kati ni 16 na viwanda vidogo ni 477.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti anasema kuwa Mkoa unaendelea na juhudi za kuwakaribisha wawekezaji wa ndani naje nchi kuja Kagera kuwekeza ambapo tayari uongozi umetenga maeneo ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda yenye ukubwa wa Hekta 58,000 katika maeneo mbalimbali kupitia kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.


Post a Comment

0 Comments