habari Mpya


Kagera yazindua Mkakati wa Kuimarsha Ulinzi na Usalama-“Nyumba Kumi Bora za Kiusalama”.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti amezindua rasmi mkakati wa kuimarisha USALAMA katika Mkoa wa Kagera uliopewa jina la “NYUMBA KUMI BORA ZA KIUSALAMA”.

Mkakati huo ukilenga kuimarsha Ulinzi na Usalama wa mkoa kuanzia ngazi ya chini katika jamii kwa kila nyumba kumi kuwa na kiongozi ambaye atakuwa na jukumu la kutambua wanafamilia wanaoishi katika kila nyumba anayoiongoza.
Mkuu wa Mkoa Gaguti ambaye ni Mhasisi na Mwanzilishi wa Mkakati huo wa kukomesha UHALIFU, UJAMBAZI NA VITENDO VYA UVUNJIFU WA AMANI katika Mkoa wa Kagera alizindua Mkakati huo kimkoa wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” wenye kaulimbiu isemayo: 10 BORA! Usalama wa Nchi, katika Kijiji cha Chabuhola, Kata Nyakabanga Tarafa Nyakakika Wilayani Karagwe Novemba 1, 2018.

Akitoa ufafanuzi namna mkakati wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” utakavyofanya kazi Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaeleza wananchi waliofurika katika hafla fupi ya uzinduzi kijijini Chabuhora Wilayani Karagwe kuwa Mkoa wa Kagera bado haufanyi vizuri katika suala la ulinzi na usalama hasa watendaji wa Serikali katika ngazi za chini hawawajibiki ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao katika suala zima la kiulinzi.

Katika Mkoa wetu wa Kagera bado tuna changamoto kubwa ya kiusalama hadi kufikia mwezi Septemba 2018 Mkoa ulikuwa na kesi za mauji 107, katika Kata hii tu tuliyopo hapa sasa ya Nyakabanga kufikia Septemba 2018 kulikuwa kumebainika wahamiaji haramu 997 na bado tunalo tatizo la magendo. Haya mambo makuu matatu yanonesha vyema kuwa bado tuna changamoto kubwa ya Kiusalama katika Mkoa”. Alieleza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa inashangaza sana kuona Mkoa wa Kagera wenye wasomi wengi na bado ni Mkoa unaoendelea kufanya vizuri katika Sekta Elimu lakini bado wananchi wake wanashiriki katika imani potofu na kupelekea kushiriki katika vitendo vya mauaji na kuifanya Kagera kuwa kati ya Mikoa ambayo inaongoza kwa vitendo vya mauaji.

Jukumu la Ulinzi na Usalama si jukumu la Vyombo vya Ulinzi na Usalama tu bali ni jukumu la kila mwananchi kulinda usalama wake mwenyewe na Usalama wa nchi na jukumu la Vyombo vya Ulinzi na Usalama ni kuongoza katika juhudi za kiulinzi na kiusalama pale panapotokea uvunjifu wa amani. 

Mwananchi mmoja mmoja anatakiwa kulinda usalama popote pale anapokuwa katika nchi ya Tanzania.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa Mkoa wa Kagera unatakiwa kuwa mbele sana katika suala la kiusalama kwani unapakana na nchi jirani nne kati ya nchi nane zinazopakana na nchi ya Tanzania. 

Mtu akiingilia hapa Nyakabanga anajifanya mwenyeji na mwisho wa siku anatupigia bao Dodoma katikati ya nchi akishafika huko anajifanya ametokea Chabuhora Nyakabanga Karagwe kumbe mhamiaji Haramu.” Alifafanua Mhe. Gaguti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bw. Godfrey Mheluka akito taarifa kwa Mkuu wa Mkoa alisema baada ya Wilaya ya Karagwe kupewa heshima ya kuzindua Mkakati wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” Uongozi wa Wilaya uliamua kufanya uzinduzi huo katika Kata ya Nyakabanga kwasababu kata hiyo inaongoza kwa mauaji na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani na mkakati huo ulizinduliwa hapo kuanza kukomesha vitendo hivyo.

Post a Comment

0 Comments