habari Mpya


Waziri Lugola –Na ziara Kigoma kusikiliza Kero .

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Polisi Katoro mkoani Geita  na kuwahoji watuhumiwa wa makosa mbalimbali waliokuwepo katika mahabusu kituoni hapo.

Waziri Lugola ambaye alikua safarini kuelekea Mkoani Kigoma kwa ziara yake ya kikazi, ghafla aliibukia katika kituo hicho akitaka kujua utendaji kazi wa polisi pamoja na makosa mbalimbali wanayowakabili watuhumiwa waliopo katika mahabusu hiyo na pia kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili askari wa kituo hicho.

Waziri Lugola aliowasili kituoni hapo jana mchana na akaelekea moja kwa moja mahabusu na akaomba kitabu cha taarifa ya makosa mbalimbali yaliyoripotiwa kituoni hapo, na akamuelekeza askari wa zamu awapange foleni watuhumiwa hao ili aweze kuwahoji makosa yao na pia Mkuu wa Kituo cha polisi hicho, aweze kufafanua makosa yao.

Baada ya watuhumiwa hao, Waziri Lugola licha ya kuwapongeza polisi wa kituo hicho kwa kufanya kazi vizuri, pia alimtaka Mkuu wa Kituo hicho, Steven Kimaro kua makini na utendaji wake na kuwafuatilia kwa umakini utendaji kazi wa askari wake kwasababu yeye ndio kiongozi wa kituo hicho.

“Sipendi wananchi waonewe, haki itendeke na si kila kosa lazima mtuhumiwa awekwe mahabusu, tumieni busara umakini ili tuweze kutenda haki na pia nataka jeshi hili liwe na picha nzuri zaidi kwa jamii,” alisema Lugola.

Pia alifafanua kua, hataki kusikia askari polisi anatuhumiwa kwa rushwa au kunyanyasa wananchi, na endapo taarifa hizo zitamfikia basi atahakikisha askari huyo anachukulia hatua za kisheria.

Aidha, Waziri Lugola alitaka polisi wa usalama barabarani kufuata sheria na pia si kila kosa lazima mwenye gari kuandikiwa risiti ya malipo, makosa mengine watoe elimu zaidi kwa madereva hao ili taifa liweze kusonga mbele.

Waziri Lugola, leo  Septemba 25 anatarajia kuanza ziara yake ya kutembelea mikoa yote nchini, ambapo ataanza ziara katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo atazungumza na askari na maafisa polisi, watumishi wa taasisi zilizopo katika wizara yake na baadaye atafanya mkutano wa hadhara kwa kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao mjini humo. 

Post a Comment

0 Comments