habari Mpya


Waziri Issack Kamwelwe asema Mazishi ya waliopoteza maisha kwenye MV.Nyerere yatafanyika Kitaifa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe amesema uokoaji wa miili ya waliofariki dunia baada ya kuzama kwa kivuko cha MV.Nyerere utakamilika leo Septemba 21, 2018 kabla ya saa 12 jioni.

ametoa kauli hiyo leo mchana wakati akihojiwa na kituo cha Utangazaji cha Taifa (TBC), akiwa eneo la tukio Kisiwa cha Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Mpaka sasa miili zaidi ya 125 imepatikana katika ajali hiyo kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella.

Mhandisi Isack Kamwelwe amesema mazishi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya Mv.Nyerere iliyotokea Septamba 20 huko kisiwani Ukara, Ukerewe mkoani Mwanza yatakuwa ya kitaifa ambapo viongozi wakuu wa kitaifa wanatarajia kushiriki mazishi hayo.

Kamwelwe amesema shughuli za mazishi hayo zitagharamiwa na Serikali na kwamba utaratibu kamili wa eneo yatakapofanyika mazishi hayo utatolewa baadaye.
Vikosi vya uokoaji mkoa wa Mwanza vimeongezewa nguvu na vikosi vya mkoa wa Mara katika eneo la tukio ili kuongeza kasi ya kuopoa miili ya watu waliopinduka na kivuko hicho.

Aidha uongozi wa wakala wa meli mkoa wa Mwanza umetambua wafanyakazi wa kivuko watano ambao wamepoteza maisha akiwemo   nahodha, fundi, Karani, mlinzi na mkuu wa kivuko, Kivuko hicho kilikuwa na wafanyakazi wanane.
Mamia ya wakazi wa Ukerewe wamekusanyika nje ya kituo cha afya cha Bwisya kutambua miili iliyoopolewa kwenye ajali ya kivuko cha MV.Nyerere iliyotokea wakati wakisafiri kutoka kisiwa cha Bugorora kwenda Ukara kwenye gulio.

Post a Comment

0 Comments