habari Mpya


Wawekezaji Ngara,Kutoa Ajira za Kudumu kwa Watanzania 2500.

Picha Na Shaban Ndyamukama -RK Ngara.

FRIIUP COMPANY (T) LTD ya Nchini Korea Kusini yaahidi kutoa ajira za kudumu kwa watanzania wapatao 2500, wakati itakapoanza shughuli zake rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera katika kipindi cha miezi tatu ijayo.

 Mkurugenzi Mtandaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Bw. Aidan J. Bahama, amesema hayo baada ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara na wa kampuni ya FRIIUP COMPANY (T) LTD ya Nchini Korea Kusini, kusaini mkataba wa kuwekeza katika kilimo.

“Jana Septemba 03, 2013 tumesaini mkataba wa miaka 10 wa uwekezaji niseme kwamba, ni uwekezaji mkubwa katika mambo mbalimbali; katika kahawa, mpunga na uwekezekaji kwenye zao la parachichi.” Alisema Bw. Bahama.

Bw. Bahama amesema uwekezekaji huo utachukua ekari takribani 12, 000, na awamu ya kwanza utagharimu dola za kimarekani zipatazo dola milioni 5, ambazo karibu ni sawa na shilingi bilioni 13  za kitanzania.
Aidha  mradi huo utakuwa na faida kwa Halmashauri, Wananchi wa Wilaya ya Ngara pamoja na Watanzania; na kwamba wameahidi kuiwezesha Halmashauri ya Wialaya ya Ngara katika miundombinu  ya barabara, hospitali, pamoja na elimu.

“Tayari konteina moja la kompyuta linakuja kwa ajili ya kuzigawa mashuleni; kompyuta hizo zinatupa uhakika wa watoto wetu kujifunza somo la TEHAMA; kwa hiyo unaweza kuona jinsi uwekezaji huo utavyokuwa na faida kubwa kwetu sisi kama halmashauri.” Alisema Bw. Bahama.

Aidha, amesema kwamba watu wanaozunguka mradi huo, watawezeshwa katika teknolojia ya kuzalisha kahawa, avocado, makademia na mpunga, ili waweze kuazalisha zaidi, huku wakiwa na soko la uhakika.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele, amewakaribisha wawekezaji katika Wilaya ya Ngara, huku akidai kwamba  ni matumaini yake kuwa wataendelea kuja ngara, ili kuhakikisha kwamba mkataba huo unatekelezwa kwa mafanikio ya wananchi wa wilaya ya Ngara.

Aidha, amefafanua kwamba wenyeji wanaozunguka mradi huo, watajifunza utaalamu mpya wa kuzalisha mazao ya biashahara kama vile kahawa, mpunga na parachichi na kusaidia kutoa mbegu bora za mazao hayo kwa wananchi wa wilaya ya Ngara.
Baada ya Serikali ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera kusaini mkataba huo imeelezwa utekelezaji wa miradi iliyopangwa utaanza miezi mitatu ijayo na kuanza kuajiri wananchi wenye sifa mbalimba kitaaluma ili kuharakisha malengo uwekezaji huo.

Post a Comment

0 Comments