habari Mpya


Vyeti Vya Kuzaliwa Kwa Watoto Chini ya Miaka Mitano Kagera Vyapatiwa Ufumbuzi na Serikali.

Na: Sylvester Raphael.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) yaja na Mpango Mkakati wa kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa sasa na wale ambao tayari wamezaliwa chini ya umri wa miaka mitano wanapata Vyeti vya Kuzaliwa kwa mfumo mpya wa Wakala (RITA) kupeleka huduma hiyo ya utoaji vyeti katka ngazi ya Vituo vya Afya pamoja na ngazi ya Ofisi za Watendaji wa Kata.

Mpango Mkakati huo wa RITA uliwasilishwa (Septemba 14, 2018) katika semina ya siku moja iliyofanyikia katika Ukumbi wa Hoteli ya Kolping Manispaa ya Bukoba ili kuwaelimisha Viongozi wa Mkoa na Wilaya kuhusu utaratibu mpya wa utoaji Vyeti vya Kuzaliwa  kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Kagera.

Akitoa maneno ya utangulizi katika Semina hiyo Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu RITA Bi. Emmy Kalomba Hudson alisema kuwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umeamua kuja na Mpango Mkakati wa kupeleka huduma ya utoaji vyeti kwa watoto chini ya miaka mitano katika ngazi ya Kata na Vituo vya Afya ili kuondoa kero zilizokuwepo awali kwasababu ya vyeti hivyo kupatikana katika Ngazi ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya tu.

Serikali kupitia RITA imeanza kufanya maboresho ya jumla ya mfumo  mzima wa usajili chini ya Mkakati wa Kitaifa wa Kuboresha Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu  na Takwimu. (National Strategy on Civil Registration and VitalStatistics). Mkakati wa CRVS una mipango mbalimbali ya utekelezaji ikiwa ya muda mfupi na mrefu kwa makundi yatokanayo na umri ili kufikia ufanisi unaotarajiwa.” Alifafanua Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Bi. Emmy Kalomba.

RITA wamekuja na Mpango Mkakati wa kusajili watoto chini ya miaka mitano baada ya Tanzania kuwa na asilimia 13.4% ya usajili ambapo kiwango hicho ni cha chini sana ukilinganisha na mataifa mengine Barani Afrika . Aidha, kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa Mkoa wa Kagera una watoto waliochini ya umri wa miaka mitano 542,806 (NBS 2018)  na watoto wenye vyeti ni asilimia 12.4% ambapo  kwa Sensa ya mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 12.2%  na watoto ambao hawajasajiliwa ni 475,498.

Akifungua Semina hiyo ya siku moja Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aliwataka wajumbe wa semina hiyo kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo na kutoa maoni ya kuboresha mkakati wa RITA katika kuhakikisha unafanikiwa katika maeneo yao na kuwa na tahadhari juu ya Wananchi wasiokuwa raia wa Tanzania kutokana na Mkoa wa Kagera kuwa na mipaka mingi na nchi jirani.

Wakiboresha Mkakati wa RITA wa kusajili watoto chini ya umri wa miaka mitano katika Semina hiyo wajumbe walipendekeza kuwa uwepo pia mpango wa kusajili miaka 5  hadi 18 kwasababu bado hitaji ni kubwa katika jamii la upatikanaji wa Vyeti vya Kuzaliwa. 

Kuzingatia suala la ulinzi na usalama wa nchi katika zoezi hilo kwa kuanzisha usalama wa nyumba kumi ili kila mwananchi ktambulika kisawasawa katika nyumba kumi.

Vigezo vya Mtoto anayesajiliwa kupitia Mpango wa Usajili wa watoto

Kwanza, Mtoto awe amezaliwa katika ardhi ya Tanzania Bara (Bila kujali uraia wa wazazi wake). Pili, Mtoto awe na umri usiozidi miaka mitano. 

Tatu, Mtoto awe na kiambatisho kimojawapo kati ya vifuatavyo: (Tangazo la kizazi au Kadi ya Kliniki.

 Nne, Vitambulisho vya wazazi (Kimojawapo kwa kila mzazi kati ya vifuatavyo, Kadi ya kupiga kura au Kitambulisho cha Taifa)

Namna zoezi litakavyendeshwa Mkoani Kagera.

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) utaendesha mafunzo ya siku tatu  kwa Maafisa sita (Afisa Ustawi wa Jamii, Mipango, Tehama, Maendeleo ya Jamii, Ugavi na Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto) kutoka kila Halmashauri ya Wilaya ili kujifua namna ya kutekeleza zoezi la usajili watoto chini ya miaka mitano katika Vituo vya Afya na Ofisi za Afisa Watendaji wa Kata.

Vvyeti vya Kuzaliwa vitakavyotolewa katika zoezi hilo vitakuwa vya kuandika kwa mkono tofauti na vinavyotolewa kwa kuchapwa na mshine lakini vitakuwa halali na vitakuwa vimesajiliwa katika mfumo wa Serikali. 

Zoezi hilo litaanza rasmi Oktoba Mosi, 2018 na litaendeshwa kwa wiki mbili lakini pia baada ya wiki hizo mbili kuisha zoezi litakuwa endelevu kwa kila mtoto atakayezaliwa.

Ikumbukwe kuwa hakutakuwa na gharama yoyote ya Cheti cha Kuzaliwa kwa mtoto chini ya umri wa miaka mitano wazazi wanatakiwa kuwapeleka watoto katika vituo watakavyokuwa wameelekezwa katika Halmashauri zao. 

Aidha, kwa uataratibu huu mpya watoto chini ya miaka mitano vyeti vyao havitatafutwa tena katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya bali wale wenye umri kuanzia miaka mitano na kuendelea.

Post a Comment

0 Comments