habari Mpya


RC Kagera atoa Siku 7 kwa KCU 1990 LTD na KDCU LTD Kurejesha Milioni 483 za Wakulima.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ameagiza Jeshi la Polisi na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera kuvisimamia Vyama Vikuu vya Ushirika vya KCU 1990 Limited na KDCU Limited kurejesha fedha za Wakulima shilingi milioni 483 ambazo zimetumika kinyume na utaratibu uliopangwa.

Gaguti ametoa agizo hilo leo Septemba 6, 2018 ofisini kwake mara baada ya kupata taarifa kuwa Vyama hivyo Vikuu viwili vilikopa fedha hizo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa ajili ya kuwalipa wakulima kutoka kwenye Vyama vya Msingi lakini Vyama hivyo Vikuu vimezitumia fedha hizo kinyume na malengo.
 “Nimepata taarifa kuwa Vyama hivi viwili vimetumia shilingi milioni 483 kwa kujilipa mishahara na kuwalipa wazabuni wakati fedha hizo zilikopwa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa ajili ya kuwalipa Wakulima kutoka Vyama vya Msingi, uongozi wa Mkoa haukubaliani na suala hili.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kuanzia saa 2:00 asubuhi kuvisimamia Vyama Vikuu hivyo viwili kufanya kazi chini ya yao kwa masaa 24 na taarifa kutolewa fedha zilitumika vipi na fedha hizo ziwe zimerejeshwa ndani ya siku saba.

Chama Kikuu cha KCU 1990 Limited kimetumia Shilingi Milioni 206 na KDCU Limited kimetumia Shilingi Milioni 282.

Post a Comment

0 Comments