habari Mpya


Chukua Hatua kwa Wakuu wa Shule Ambao Hawajakamilisha Maabara

Mheshimiwa Mkurugenzi chukua hatua kwa Wakuu wote wa Shule za Sekondari waliopewa fedha za kukamilisha Maabara na hawajakamilisha shughuli hiyo, hatuwezi kuvumilia wakuu  wanaokwamisha utekelezaji wa shughuli za serikali.” Kaagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele.

Lt. Col. Mntenjele alitoa agizo hilo wakati wa Baraza la Madiwani, lililofanyika Agosti 29, 2018 katika ukumbi wa Halamshauri ya Wilaya ya Ngara kufuatia tuhuma zilizotolewa na Madiwani kuhusu Maabara za Shule ya Kanazi na Murugwanza kujengwa chini ya kiwango.

Amesema kwamba katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali changamoto haziwezi kukosa, akawaagiza Waheshimiwa Madiwani kusimamia kwenye maeneo ambayo yana changamoto ili isije kuonekana hata Viongozi ni sehemu ya kukwaza kazi hizo.

Akitoa mfano, Lt. Col. Mntenjele amesema Shule ya Sekondari ya Kanazi imepewa milioni 19 ya kukamilisha Maabara, lakini kilichofanyika pale ni sawa na ziro na kwamba Shule za Sekondari nyingine zimefanya kazi nzuri kwani Maabara zao Zimekamilika kwa Wakati.

Ukienda katika shule nyingine zilizopewa fedha za kukamilisha maabara zinapendeza unaona kweli kazi imefanyika, na  kwa kweli unasema kama watoto wakishindwa mitihani yao ya sayansi anakuwa ni yeye mwenyewe kwani mazingira yanaruhusu watoto wasome.” alisema Lt. Col. Mntenjele.

Alisema hatutaeleweka kama Serikali inaleta fedha kwa ajili ya kufanyakazi, halafu kazi haionekani, inasikitisha sana na kuongeza kwamba uzembe huo unawakwamisha watoto kufanya vizuri.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Bw. Aidan  Bahama ametekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele kwa kuwaagiza Mkaguzi wa Ndani na TAKUKURU kufanya ukaguzi katika shule ya sekondari za Kanazi na Murugwanza.

Amewataka kukagua kwa kina matumizi ya fedha waliyopewa na wamletee ripoti; “Nendeni pale kagueni matumizi ya fedha iliyotolewa kisha mniletee ripoti nikishapata taarifa zote mbili nitazisoma kisha nitachukua hatua stahiki.” Alisema Bw. Bahama.

Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Bw. Erick Nkilamachumu amesisitiza kwamba mkaguzi wa ndani na ofisi ya TAKUKURU wamepewa kazi ambayo inabidi waifanye haraka iwezekanavyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Mmepewa kazi tusaidieni kama mtu amepewa milioni tano basi kazi iwe ya milioni tano siyo mtu anapewa milioni tano kazi hata haishabiiani na kiwango cha fedha alichopewa.” alisema Bw.Nkilamachumu.

Post a Comment

0 Comments