habari Mpya


Taarifa ya DC Bukoba kuhusu Kifo cha Mwanafunzi aliyefariki kwa kipigo cha Mwalimu.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawiro kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ametoa taarifa ya Serikali juu ya kifo cha Mwanafunzi Spelius Eladius (13) wa Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba anayesadikiwa kufariki dunia baada ya kupigwa na Mwalimu Respecius Mutazangira ambaye ni Mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo ya Kibeta kwa kutuhumiwa kuiba pochi ya Mwalimu Elieth Gerald.

 Mkuu wa Wilaya Deodatus Kinawiro akitoa taarifa ya Serikali kwa Vyombo vya Habari leo Agosti 29, 2018 alisema kuwa mara baada ya tukio hilo kutokea siku ya Jumatatu Agosti 27, 2018 Serikali ilichukua hatua mara moja kwa kuwakamata watuhumiwa wanaotuhumiwa kufanya kitendo hicho ambao ni Mwalimu Respecius Mutazangira (anayetuhumiwa kumpiga mtoto na kumuua), Mwalimu Elieth Gerald (aliyetoa taarifa kuwa amebiwa pochi yake) pamoja na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo.

Baada ya kuwakamata watuhumiwa hao Jeshi la Polisi Mkoani Kagera linaendelea kufanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwahoji Walimu waliokuwepo wakati tukio hilo linatokea ili kukamilisha uchunguzi wa tukioa na mara baada ya kukamilisha uchunguzi watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.
Mkuu wa Wilaya Kinawiro alitoa rai kwa wananchi hasa wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo ya Msingi Kibeta kuacha kuwazuia wanafunzi kwenda shuleni hapo kuendelea na masomo yao kwani hali tayari imetulia na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi lakini pia Serikali inaendelea kuifanyia kazi taarifa ya uchunguzi ya Kidaktari iliyotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa juu ya sababu zilizosababisha kifo cha Mwanafunzi Spelius Eladius.

Jana asubuhi siku ya Jumanne tarehe 28 Agosti, 2018 nilifika Shule ya Msingi Kibeta na kukutana na Walimu na Wanafunzi niliongea nao na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendlea kufanya kazi kuna kuwataka walimu kuendelea kufundisha na watoto waendelee kuingia madarasani. Lakini pia leo tarehe 29 Agosti, 2019 nimeenda shuleni hapo kuangalia hali lakini nimekuta kuna baadhi ya wazazi wamewazuia watoto wao kwenda shuleni, natoa wito kwa wazazi wawache watoto waende shule kwani hakuna tishio lolote shuleni hapo.” Alitoa wito Mkuu wa Wilaya Kinawiro.

Aidha, Mhe. Kinawiro alitoa wito kwa wananchi wa Bukoba kutulia na kuiamini Serikali yao kwani tukio hilo linaendelea kufanyiwa kazi na taarifa zitakuwa zinatolewa mara kwa mara na Serikali hasa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili wananchi wajue kila kinachoendelea katika kuhakikisha haki inatendeka na wananchi wanapata taarifa sahihi jinsi kifo cha mwanafunzi huyo kilivyotokea na ni nini kilisababisha kifo hicho.

Pia Mhe. Kinawiro alito wito kwa Walimu katika shule Mkaoni Kagera kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kulingana na kanuni, taratibu na sheria na kuzingatia kanuni na miongozo ya utoaji wa adhabu kwa wanafunzi watakaobainika kuwa na makosa lakini wasichukue hatua za kutoa adhabu holela bila kufauta kanuni za utoaji wa adhabu hizo na kusababisha madhara kwa wanafunzi.

Mwanafunzi Spelius Eladius (13) wa Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba anasadikiwa kufariki dunia Agosti 27, 2018 muda mfupi baada ya kupigwa viboko na Mwalimu Respecius Mutazangira Mwalimu wa shue ya Msingi Kibeta na kusabisha kifo chake baada ya mwanafunzi huyo kusadikiwa kuwa ameiba pochi ya Mwalimu Elieth Gerald asubuhi alipompokea Mwalimu huyo mizigo yake lakini baadae ilikuja kugundulika kuwa hakuwa ameiba pochi hiyo. 

Uchunguzi wa suala hili unaendelea na taarifa zitatolewa na Serikali kadri suala hili linavyofanyiwa kazi.

Post a Comment

0 Comments