habari Mpya


RC Kagera aridhishwa na ujenzi wa shule ya Ihungo unaoendelea baada ya kufanya ziara katika shule hiyo.

Na: Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti atembelea Shule ya Sekondari Ihungo na kuona maendeleo ya ukamilishwa wa baadhi ya miundombinu midogomidogo katika majengo baada ya Serikali kuamua na kuijenga upya shule hiyo iliyoharibiwa vibaya na Tetemeko la Ardhi lililotokea Mkoani Kagera Septemba 10, 2016

Mkuu wa Mkoa Gaguti mara baada ya kufanya ukaguzi na kuridhishwa na ujenzi wa shule hiyo Agosti 25, 2018 alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuri kwa kufanya uamuzi sahihi wa kujenga upya shule hiyo ya Ihungo na kukarabati baadhi ya majengo  kwa gharama ya shilingi bilioni 10.45 na kuifanya shule hiyo iwe shule bora na ya kisasa nchini inayovutia elimu bora kwa wanafunzi.

Mara baada ya Shule ya Sekondari Ihungo kukamilika ujenzi wake kwa asilimiazaidi ya 90% Serikali tayari imewarudisha wanafunzi walikokuwa wamehamishiwa katika Shule ya Sekondari Omumwani Manispaa ya Bukoba na Chuo cha Ruhija Halmashauri ya Wilaya Bukoba ili wakaendelee na masomo yao katika shule yao ya Ihungo Sekondari.
Katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu midogo midogo iliyobakia katika katika shule hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mkoa Gaguti alisema kuwa yeye jukumu lake ni kufuatilia na kuhakikisha kila kilichopangwa kujengwa katika shule hiyo lazima kijengwe na kukamilshwa na Kampuni ya Tanzania Building Agency (TBA).

Tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera lilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu yote ya Shule ya Sekondari Ihungo  ikiwemo Madarasa, Mabweni, Maabara, Bwalo, Jiko, Vyoo na Mabafu, Nyumba za Walimu, Jengo la Utawala, Kanisa, Msikiti, Maktaba na Mifumo ya maji na umeme. 
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga majengo matatu ya madarasa yenye ghorofa moja kila moja, kila jengo lina vyumba 8 vya madarasa na ofisi 4 na kufanya jumla ya vyumba vya madarasa 24 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 960 na jumla ya ofisi 12.
Serikali pia imejenga majengo 3 ya mabweni yenye ghorofa 2 kila moja, kila jengo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 384; hivyo majengo yote 3 ya mabweni yatachukua wanafunzi 1,152, vikiwemo vyoo na mabafu. Serikali pia inajenga nyumba mpya za wafanyakazi kwa matumizi ya familia 30.

Aidha, Serikali imefanya ukarabati wa Maktaba ya Shule, Jengo la Utawala, Maabara ya Kompyuta, Jengo la Kilimo, Bwalo, Jiko na Maabara za Fizikia, Kemia na Baologia.

Tayari Shule ya Sekondari Ihungo imepangiwa wanafunzi 679 wa Kidato cha Tano na tayari wanafunzi  556 wameripoti shuleni hapo tangu tarehe 16/7/2018 na wanafunzi hao ni wa michepuo ya PCB, PCM, CBG, EGM na HGE  na wanaendelea na masomo kadri ratiba ya shule ilivyopangwa.


Pamoja na changamoto za Tetemeko la Ardhi kuiharibu vibaya shule ya Ihungo Sekondari lakini wanafunzi na Walimu hawakukata tamaa kabisa bali walijifua vizuri na shule hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa  ya Kidato cha Sita mfano mwaka 2017 kati ya wanafunzi 372 waliofanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita 54 walipata dalaja la kwanza, 133 daraja la pili, 167 daraja la tatu, 15 daraja la nne na watatu walipata sifuri.

Mwaka 2018 kati ya wanafunzi 364 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato Sita 43, walipata dalaja la kwanza, 160 daraja la pili, 151 daraja la tatu, 8 daraja la nne na wawili walipata sifuri. Ikumbukwe kuwa Shule Sekondari Ihungo awali kabla ya Tetemeko kutokea ilikuwa ina uwezo wa kubeba wanafunzi 801 na kwasasa baada ya kujengwa upya inao uwezo wa kubeba wanafunzi 1,152.

Post a Comment

0 Comments