habari Mpya


Mkuu wa Mkoa Gaguti Aweka Jiwe la Msingi Mradi wa Barabara wa Bilioni 7.3 Manispaa ya Bukoba.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Marco E. Gaguti aweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami nzito zenye urefu wa kilometa tano katika Manispaa ya Bukoba ambapo mradi huo utagharimu jumla ya shilingi bilioni 7.3 utakapokamilika Mwezi April 2019.

Mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika eneo la mradi Nshambya kwenye kipande cha barabara chenye kilometa 1.7 Mkuu wa Mkoa Gaguti alimtaka Mkandarasi NCL INTERNATIONAL LIMITED kutekeleza mradi huo kwa kiwango kinachotakiwa na kuukamilisha kwa muda uliopangwa au ikiwezekana aukamilishe kabla ya muda ili wananchi wawanufaike na mradi huo mapema zaidi.
Pia Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanausimamia mradi huo pamoja na kuwa na wasimamizi wataalamu lakini pia wananchi wana wajibu wa kutoa taarifa  watakapoona hawaridhishwi na kazi zinazotekelezwa na Mkandarasi watoe taarifa mara moja kwani mwisho wa siku mradi huo utabaki kuwa wa kwao na ndio wanufaika.

Vilevile Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwahasa wananchi katika mambo makuu mawili ya msingi ambapo jambo la kwanza aliwaasa kufanya kazi kwa bidii sana ili kujiingizia kipato.
Aidha, Mhe. Gaguti aliwahakikishia wananchi kuwa atashughulikia kero kwa wajasiliamali mbalimbali hasa Waendesha pikipiki (Maarufu Bodaboda) ili waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri na kulipa kodi za Serikali.

Jambo la pili alilowaasa wananchi ni kuwa atahakikisha anasimamia  kwa karibu sana ulipwaji wa  kodi za Serikali kwa kila anayetakiwa kulipa iwe mwananchi mmoja mmoja,Taasisi au Kampuni ili Mkoa wa Kagera uweze kuongoza katika ulipaji wa kodi za Serikali kama unavyoongoza kwa kushika nafasi za juu katika elimu ili fedha hizo zirejeshwe na kufanya shughuli za maendeleo ya wananchi.

Mradi wa ujenzi wa barabara katika Manispaa ya Bukoba umegawanyika katika sehemu kuu nne ili kukamilisha kilometa tano ambapo kilometa 1.7 ni barabara ya Nshambya KCDP itakayogharimu zaidi ya  shilingi bilioni 2.1 

Aidha, kuna kipande cha Show kilometa 1.05, Nyangoye kupita Halmashauri ya Bukoba (Chemba) kilometa 1.3 na kipande cha kilometa 1.95 cha Bin Said hadi Kilimahewa. 

Barabara zote zenye urefu wa jumla ya kilometa 5 zitagharimu jumla ya shilingi bilioni 7.3.

Fedha za kutekeleza mradi huo wa kuimarisha miundombinu ya barabara mijini ilitolewa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo muda wa utekelezaji wa mradi ni kuanzia Juni 18, 2018 hadi Aprili 17, 2019 ambapo kazi ziatakazofanyika ni kujenga makaravati 17, mifereji ya maji, kuweka rami nzito na kujenga daraja moja eneo la barabara ya kuelekea ziwani.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkao Gaguti alitembelea kiwanda cha BUKOP cha kukoboa kahawa kujionea ukoboaji wa kahawa unavyoendelea, Pia litembelea mradi wa BUWASA wa upanuzi wa huduma za maji Ihungo  na kukagua Ujenzi wa madarasa yaliyofadhiliwa na Serikali ya Watu wa Japani katika Shule za Msingi Kashozi na Nyakato Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, mwisho aliongea na kujitambulisha kwa watumisha wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na Manispaa ya Bukoba na wadau mbalimbali wa maendeleo katika ukumbi wa chemba Bukoba Vijijini.

Post a Comment

0 Comments