habari Mpya


Mfahamu wanafunzi aliyeongoza matokeo ya kidato cha sita kitaifa 2018

SHAABAN NDYAMUKAMA, RK NGARA.
Mhitimu wa kidato cha sita aliyeongoza matokeo  kitaifa kutoka shule ya sekondari Mzumbe mkoani Morogoro Anthony Karugendo Mulokozi (20)  amesema ndoto ya maisha yake ni kuwa daktari wa binadamu   akilenga kuwasaidia watanzania wanaohitaji huduma za kiafya.

Mulokozi amebainisha hayo jana nyumbani kwao   katika  mtaa wa Murutambikwa ulioko mamlaka ya mji wa Rulenge wilaya ya Ngara mkoani Kagera  wakati akiongeza na Radio Kwizera na kwamba alipata msukumo wa kupenda kuwa daktari kutokana na ushindi wa masomo ya sayansi  kuanzia elimu ya msingi
Picha juu ni kijana Anthon Mulokozi akiwa na baba yake Julius Karugendo nyumbani kwao Rulenge Ngara. 
Mulokozi amesema  anahitaji kuwasaidia watanzania wanaokabiliwa na changamoto za afya  baada ya kujifunza mfumo wa mwili wa binadamu akiwa shule ya msingi Rhec English Medium iliyoko kata ya Rulenge wilayani Ngara.

 “Nilianza kupenda kuwa mtumishi wa afya nikifuata nyayo za mama mzazi aliyekuwa muuguzi wa Hospitali kabla ya kuacha  alipohudumia mashamba na mifugo akisaidiana na baba hadi leo napenda fani hiyo” Alisema Mulokozi
Aidha alisema alipata msukumo wa kupenda kuwa daktari kutokana na ushindi wa masomo ya sayansi na kupewa motisha baada ya matokeo ya darasa la saba kuwa mshindi wa kwanza katika wilaya ya Ngara alipochaguliwa kwenda Tabora boys

Pia alisema   matokeo ya kidato cha nne alipata  daraja la kwanza  point inane  na katika masomo ya kidato cha sita  kwa wanafunzi 121 alikuwa akipata nafasi ya tatu hadi ya kwanza kwenye mitihani ya ndani .

“Natamani wakati wa masomo ya Chuo Kikuu niwe miongoni mwa wanafunzi watakaopata nafasi ya kwenda nje ya nchi kujifunza zaidi uchunguzi wa kisayansi kuhusu mwili wa binadamu na maradhi yake” Aliongeza Mulokozi
Anthony Mulokozi alizaliwa Juni 14, 1998, alijiunga na elimua ya msingi mwaka 2005 hadi 2011 kisha kujiunga na sekondari ya wavulana Tabora mwaka 2012 mpaka 2016 na kuchaguliwa kwenda Mzumbe Sekondari kwa masomo ya PCB
MAMA MZAZI WA ANTHON MULOKZI ANGELA KARUGENDO.
Aidha wazazi wake ambao ni  Julius Kalugendo na Angella Kalugendo  wakazi wa   Rulenge, wamefurahia  kijana wao kuwa mshindi wa matokeo hayo kitaifa baada ya kuwa msikivu na mwenye kuzingatia malezi na maadili ya kiroho na kijamii.

Walisema  mtoto wao huyo ni kizazi cha tatu kati ya watoto wanne ambaye ameonekana kujihusisha sana na masomo ya kisayansi lakini pia akiwa msikivu aliyeweza kuwa mwaminifu wa matumizi ya rasilimali fedha  katika  masomo
“Kipato cha familia ni cha wastani kutokana na kujihusisha na kilimo na ufugaji ambapo tulitumia kipato kidogo hiki kuwasomesha watoto wote wanaendelea vema kitaaluma wakifutama malezi ya familia na walimu wao” Alisema Angella
Kalugendo alisema alimwamini kijana wake kufanya vizuri baada ya kushinda mtihani wa kujiunga na seminari ambapo mapadre walimuhitaji sana kutokana na unyenyekevu wake  lakini hakwenda seminari alijiunga na shule za serikali.

 “Nawashukuru sana waliomuona mwanagu na kumsaidia kimasomo na kiroho katika imani yake , lakini pia nampongeza kwa kushirikiana na wananfunzi wenzake darasani hadi akawa na ushindi alioupata” Alisema mzee Kalugendo
Pia  alimshauri kuzingatia maadili ya kifamilia ya upendo kwa watu , kuendelea kumuabudu na kumuomba mungu katika safari yake ya kimasomo na kujihadhari na makundi ya kijamii ambayo yanaweza kuharibu ndoto za maisha yake

Baba mzazi wa Anthony Kalugendo Mulokozi  ni Afisa mifugo wa kata Kata ya Rulenge wilayani Ngara akijihusisha na ufugaji wa kuku wa mayai akiwauzia wenye mahitaji  ambapo mifugo kama mbuzi na ng’ombe hutumika kuwasomesha watoto wake wanne wanaoendelea na masomo hapa nchini .

Mama mzazi alikuwa  Muuguzi  msaidizi wa Hospitali ya Rulenge lakini kutokana na changamoto za maisha aliamua kuacha kazi na kusimamia miradi ya kilimo na ufugaji akilea watoto wake ambao ni wa  kiume watatu wa kike mmoja.

MWANAFUNZI ERIKA ERICK ALIYESOMA SHULE YA MSINGI RHEC NA ANTHON KARUGENDO.
Vilevile mmoja wa wanafunzi waliosoma na Anthony katika shule ya msingi Rhec aitwaye Erica Erick Ntamuti ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari Zanaki alisema walikuwa na ushirikiano kwa kusoma kwa bidii
 “Tulikuwa  shule  tofauti  elimu ya sekondari lakini tuliendelea kuwasiliana na kupeana moyo wa kujifunza mpaka sasa tunajivunia kudumisha upendo na kushauriana kujihadhari na makundi yasiyokubalika kijamii” Alisema Ntamuti
Alisema jambo la msingi ni kuzingatia maadili mema, maelezo ya wazazi jamii na serikali lakini pia kulenga ndoto za maisha yao kufanikiwa ambapo yeye analenga kuwa mkalimani  wa lugha ya kifaransa na kiingereza akihitimu chuo kikuu.HERENA ADRIAN GOZI AKIWA NA MWANAFUNZI WAKE ANTHON KARUGENDO.
Mwalimu wa elimu ya awali  hadi darasa la saba katika shule ya Rhec English Medium Helena Adrian ambaye ni Meneja wa shule hiyo alisema Kijana Anthony alipenda kujifunza akishirikiana na wenzake shuleni hapo   alipoanza masomo
Alisema katika kila darasa alikuwa akiongoza kwa kuwa mshindi wa kwanza au wa pili kila mwaka na kujinyakulia zawadi mbali mbali za masomo yakiwemo ya sayansi akiwa kinara wa maonesho ya kujieleza akifundisha wenzake darasani
“Amekuwa kiongozi wa kuigwa shuleni hapa aliyefuata misingi ya malezi ya familia shuleni kanisa lakini alikuwa mdadisi wa kufanya uchunguzi wa kisayansi na kuwa miongoni mwa wanafunzi wanaojituma” Alisema  Helena Adrian.

Pia alisema Kalugendo  ni mwanafunzi wa pili kuwa mshindi wa masomo ya sayansi kitaifa kutoka Rulenge wilayani Ngara  baada ya mwanafunzi wa kwanza kuwa Deusdedit Kakoko ambaye ni Mkurugenzi wa Bandari  jijijini Dar es Salaa.

Kakoko alikuwa mshindi wa kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne  mwaka 1982 na aliendelea kuwa na ufaulu mkubwa katika masomo yake hadi kwenye nafasi anazozitumikia anaonesha kipaji cha ujuzi wa mambo.
Helena Adriani lishauri serikali kuwafuatilia wanafunzi wanaojiweza  kitaaluma na   kuwapatia ufadhili wa kwenda hata nje ya nchi   kuwaongezea maarifa katika kutimiza ndoto zao  kwa kusaidia wazazi wao wasiojiweza kiuchumi.Post a Comment

0 Comments