habari Mpya


Waislamu Jiandaeni na Ibada ya Hijja - Sheikh Kagimbo.

Shaaban N. Ndyamukama RK.

 Waumini wa dini ya kiislamu waliojaliwa kuwa na uwezo kiuchumi kujiandaa kutekeleza nguzo ya tano ya dini hiyo ya kwenda kufanya ibada ya hijja katika miji ya Makka na Madina katika taifa la Saudia Arabia.

Wito huo umetolewa ijumaa hii na Sheikh wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera Sheikh Zachariah Kagimbo katika ibada ya sala ya Ijumaa msikiti mkuu wa Nshamba wilayani humo.

 Skeikh Kagimbo amesema kwamba kwenda hijja maandalizi yake huanzia mwezi wa Dhulkada mwezi wa kiislamu mpaka mwezi wa Dhulhija ambapo humpiga mawe sheitwani na kunyoa nywele huku wakichinja wanyama kuashiria alichokifanya nabii Ibrahim.

 
 
"Kwenda hijja kunahitaji uadilifu kwa anayefuata maelekezo ya mafundisho ya Qur'an na sunna za mtume Mohammad bila kuwa na hitilafu baina ya Hajii na jamii inayomzunguka" Amesema Sheikh Zachariah.

 Amesema kwa wanaotaka kwenda hijja wanatakiwa kutumia fedha walizopata kwa njia halali bila kuwa na mikopo kwa watu au madeni kwani kufanya hivyo hakuswihi kulingana na mafundisho ya Mtume Mohammed SAW.

 Kwa upande wake Sheikh wa msikiti wa Udoe ulioko Kariakoo jijini Dar es Salaam Hashir bin Zachariah amesema uislamu hauna budi kutambulishwa na waumini wake wenye kuamini Mungu mmoja na Mtume wa mwisho ambaye ni Mohammad SAW katika maeneo wanakoishi. 

Amesema katika kumcha Mungu lazima wazingatie mafundisho yaliyomo ndani ya Qur'an kwa kuepuka machafuko ya kidunia kama mauaji , mipasuko ya kiimani, chuki kwa kuonesha upendo, udugu, umoja ushirikiano kulinda amani.

Post a Comment

0 Comments