habari Mpya


Ugonjwa wa Degedege wamuathili mtoto na kumfanya kudumaa kwa miaka kumi sasa wilayani Ngara mkoani Kagera.

Pichani ni mama wa mtoto mwenye ulemavu Bi.Aisha Idd akiwa na mwanae. 

Na mwandishi wetu Shaaban Ndyamukama:
Wakati yakifanyika maadhimisho ya mtoto wa Afrika kwa kupaza  sauti kuomba kupata haki zao kikatiba bado watoto wengine hawaishi  maisha ya furaha kwakukosa mahitaji muhimu na hakizao kama vile afya na elimu.


Lakini pia ukosefu wa fedha na utengano wa wazazi kutokana na majukumu ya kiserikali umemfanya mtoto mmoja katika eneo la Benako   wilaya ya Ngara mkoani Kagera kukosa matibabu baada ya kuugua ugonjwa wa kukakamaa mwili mzima aikidaiwa aliupata baada ya kuugua degedege akiwa na mumri mdogo.

Mtoto huyo  ni mlemavu aliyekakamaa viungo vya mwili hawezi kisimama, wala kuongea,kutembea na kufanya lolote, anategemea ndugu zake na mama mzazi kumpatia huduma  kama kumlisha na kumnywesha, kumsafisha baada ya kujisaidia  haja kubwa na ndogo alipolala lakini pia kumvisha nguo kumkinga na baridi.

Mama mzazi  wa mtoto huyo Aisha Idd  anasema mtoto wake mwenye  umri wa miaka 10  aliwahi kumfikisha Hospitali ya mnazi mmoja  kwao Zanzibar   kisha  kuhamia  mkoani Kagera kutokana na mumewe  kuwa askari polisi anayehamishiwa vituo mbalimbali  japo makazi yamewekwa Benaco  wilayani Ngara.

Anasema mtoto huyo amepelekwa hospitali za hapa wilayani Ngara hasa Murugwanza  lakini haoni mabadiliko na humpatia tu chakula lakini kadhoofika kwa familia kukosa fedha za kumpeleka hospitali kupata matibabu ya maradhi hayo
Mtoto wangu alikamatwa  na ugonjwa huo  ghafla akiwa na umri wa mwaka mmoja kwa ugonjwa wa degedege na kufikishwa hospitali ya Mnazi mmoja lakini hakupata unafuu wa kimatibabu na nimekuwa naye hadi hivi unavyomuona” Alisema Aisha.

Katika familia huyo mlemavu huyo ni mtoto kati ya watoto saba ingawa kati ya hao pia wapo wengine wawili mmoja wa kike (17) na kiume (20) wanaonekana kuwa na mtindio wa ubongo  kwani huyo mkubwa hushinda mitaani akicheza na watoto wadogo na kurudi usiku 

"Waliwahi kuja walimu wa shule jirani wakiorodhedha walemavu na kuleta msaada wa chakula na nguo baadaye sikuwaona tena, mwanangu huyu anakula chochote halali ispokuwa vyakula vigumu ndo hawezi" Alisema

Kilio cha mama wa mtoto mwenye ulemavu  anaomba watu wenye kujaliwa fedha wamsaidie mtoto wake  kupata matibabu katika  Hospitali na hata kupata baiskeli ya magurudumu matatu (wheelchair) aweze kupelekwa nje kuliona jua kwani maisha yake ni kukaa sebuleni kwenye kochi na uani kwenye godoro

Vile vile  Aisha aliomba serikali kumrudisha mumewe Hamisi anayefanya kazi ya askari polisi wilayani Muleba  aweze kuwa mazingira ya nyumbani ama Ngara au Zanzibar  ili washirikiane  pamoja kuwalea watoto hao ambao wanamatatizo ya kiafya na kiakili.

Kwaupande wake baba mzazi wa mtoto huyo Hamisi Shaabn amesema mpaka sasa amehangaika kwamuda mrefu katika Hospitali mbalimbali na waganga wa Tiba asili kwaajili ya kutafuta huduma za matibabu ya mtoto huyo lakini imeshindikana. 
"Nimefanya kila jitihada ili mwanangu apone nimetembea Hospitali mbalimbali na kwa waganga wa tiba asili mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote "amesema Hamisi baba wa mtoto huyo.

Dakt. Simon Kyamwenge wa Hospital ya Nyamiaga  wilayani Ngara anasema mtoto huyo akifanyiwa uchunguzi  na kubaini tatizo lake, anaweza kupata huduma za matibabu  kisha kulishwa vyakula vyenye virutubisho na kurejea hali yake ya  kawaida
"Hatuwezi kumzungumzia mgonjwa ambaye hatunaye wodini kwenye uchunguzi wa afya yake, lakini katika hali  ya kawaida amedumaa kimwili na akili akifikishwa kwa wataalam wanaweza kujaribu kumfanyia matibabu" Alisema Dr Kyamwenge. 
 
Uongozi wa kijiji cha Rwakalemela eneo la Benako  Kata ya Kasulo chini ya Mwenyekiti Braithony Kemikimba umetoa wito kwa wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum ili serikali na wadau wengine  wawasaidie  jinsi ya kuwalea.

Kaimu Mwenyekiti wa kijiji hicho Johnathan Zofilo aliitaka idara ya ustawi wa jamii wilayani humo  kutembelea viongozi  wa kijiji na mitaa kuwapatia maelekezo ya kusajili watoto wenye ulemavu  na wengineo kuepuka kufichwa au kifanyiwa vitendo vya ukatili.
 


Post a Comment

0 Comments