habari Mpya


Shirika la World Vision Tanzania lakabidhi Majengo mradi wa Izigo ADP wilayani Muleba mkoani Kagera.

Shirika la World Vision Tanzania, limekabidhi majengo yaliyojengwa na mradi wa Izigo ADP kwa kushirikiana na wananchi wa kata za Muhutwe na Katoke wilayani Muleba mkoani Kagera.

 Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Meneja wa Kanda ya Kagera, Bi Juliana Charles ameeleza kuwa, Mradi wa Izigo ADP ulianza utekelezaji wa shughuli zake mnamo mwaka 2003.

Mradi huu unafadhiliwa na nchi ya Ujerumani na unajumuisha kata nne ambazo ni Izigo, Katoke, Muhutwe na Mayondwe. Pia mradi huu umekuwa ukitekeleza miradi ya Afya, Kilimo na Mifugo(uhakika wa Chakula), Ufadhili wa watoto na miradi mwingine mtambuka kama Elimu na Maji kupitia maandiko.


Miradi iliyokabidhiwa ni Mradi wa Zahanati Bushekya uliojengwa kwa thamani ya Tsh. 80,070,730.00 ambapo World Vision imetoa kiasi cha Tsh. 76,314,410.00 na wananchi wamechangia Tsh. 3,756,320.00. 

Mradi wa pili uliokabidhiwa ni mradi wa Vyumba viwili vya madarasa Shule ya Msingi Katoke B" ambao umegharimu kiasi cha Tsh. 46,998,810.00 ambapo World Vision imechangia Tsh. 43,868,810.00 na wananchi wamechangia Tsh. 3,130,000.00.

Aidha, Meneja wa Kanda ya Kagera amemshukuru na kutoa pongezi za pekee kwa Mheshimiwa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji (MB) kwa kuunga mkono na kuchangia kwa kiwango kikubwa kwa upande wa nguvu za Jamii. Pia amekuwa akifanya kazi hii kwa miradi mingi katika maeneo mbalimbali ya jimbo na hakika bila mchango wake ile dhana ya "Community Contribution" ambayo wafadhili hutaka kuona kwanza kabla ya kukubali andiko isingewezekana.Akipokea na kufungua miradi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Ndg Emmanuel Sherembi, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Muleba amewashukuru sana Shirika la World Vision kwa kazi nzuri ya kushirikiana na Serikali katika kujenga na kuboresha miundombinu ya kutoa huduma kwa wananchi. 

Aidha, amewaomba kuendelea Shirika la World Vision Tanzania na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Post a Comment

0 Comments