habari Mpya


Picha-Walimu waendesha Mgomo baridi katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu mpaka Watakapolipwa Stahiki zao.

Na Philmon Golkanus –Radio Kwizera Kasulu.

Walimu waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda masingi katika halmashauri ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma, wameazimia kuendesha mgomo Baridi na kutofika kwenye vituo vyao walivyopangiwa, mpaka watakapopewa stahiki zao zote.

Maamuzi hayo yamefikiwa hii leo wakiwa nje ya ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kasulu Bi. Fatina Laayi wakidai kupata mwafaka juu ya malipo yao ya uhamisho ili waweze kuwajibika katika shule walizopangiwa.

Walimu hao wameiambia Radio Kwizera kuwa wamefuatilia zaidi ya miezi mitatu sasa tangu kutolewa kwa agizo hilo lakini mpaka sasa hawajapatiwa stahiki zao huku nao wakiahidi kutofika katika vituo walivyopangiwa mpaka stahiki zao zitakapolipwa.
Katibu wa Chama cha walimu (CWT) wilayani Kasulu Mwl. Buchumi Felister Nkayamba, amesema msimamo wa chama cha walimu ni kuitaka halmashauri hiyo kuwalipa walimu stahiki zao kama maelekezo ya Raisi yanavyoelekeza

Hata hivyo mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kasulu Bi. Fatina Laayi, alipoulizwa kuhusu malalamiko ya walimu hao amesema hayupo tayari kulizungumzia suala hilo ambapo radio kwizera inaendelea kufuatilia kwa ajili ya kupata majibu.

Post a Comment

0 Comments