habari Mpya


Waziri Mkuu awataka Viongozi wa Mikoa kukomesha Utoro wa Wanafunzi Shuleni.

2
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwansha Mwenge wa Uhuru kuzindua mbio zake kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018 Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama.
3
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kiongozi wa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Charles Kabeho   wakati alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita Aprili 2, 2018.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 zinaongozwa na Bw. Charles Kabeho kutoka mkoa wa Dar es Salaam akishirikiana na Bw. Issa Abasi Mohamed (Kusini Pemba), Bi. Agusta Safari (Geita), Bw. Ipyana Mlilo (Tanga), Bw. Dominick Njunwa (Kigoma) na Bi. Riziki Hassan Ali (Kusini Unguja).
8
Watoto wakionyesha halaiki katika sherehe za kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru zilizoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni.
Kwa ujumla utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni mkubwa zaidi kwa mikoa husika kuliko shule za msingi. Nitumie nafasi hii kuikumbusha mikoa niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi, walezi na wanafunzi wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio shuleni.”
Waziri mkuu ametoa agizo hilo Jana,Jumatatu April 2, 2018, wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika Uwanja wa Magogo mkoani Geita. Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Waziri mkuu amesema dhamira ya Serikali kupitia kaulimbiu hiyo ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika elimu na kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda ili nchi iwe ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Akizungumzia kuhusu utoro kwa shule za sekondari nchini, waziri mkuu amesema Mkoa wa Tabora ndiyo unaoongoza kwa utoro kwa kuwa na silimia 9.7,
Geita asilimia 8.1, Mtwara asilimia 6.4 na Shinyanga asilimia 6.3.
Kuhusu utoro wa wanafunzi wa shule za msingi nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa unaoongoza ni wa Rukwa kwa asilimia 3.2, Geita asilimia 3.1, Tabora asilimia 2.9, Simiyu asilimia 2.0 na Singida asilimia1.9. 
Amesema mikoa yenye kiwango kikubwa cha utoro wa wanafunzi na kuacha shule ihakikishe mahudhurio yanadhibitiwa shuleni ili wanafunzi wote wanaoandikishwa wahakikishwe wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu.
Ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayo heshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, lazima uwekeze zaidi katika elimu”.
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha Taifa linafikia viwango bora vya elimu, Serikali imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bibi Jenista Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa takribani kilomita 103,440.7 kwa siku 195 katika mikoa yote 31 nchini na halmashauri za wilaya 195.
1
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kiongozi wa vijana  sita watakaokimbiza Mwenge huo,Charles Kabeho wakati alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama.

Post a Comment

0 Comments