habari Mpya


Zifahamu Faida za Kula Papai.

WATU wengi hulitumia tunda la papai kwa sababu ya utamu wake lakini lina faida lukuki kwa afya ya mwanadamu.

Tunda la papai lina vitamini A,B,C,D, na E jambo linaloliweka tunda hili katika kundi la matunda na vyakula vyenye utajiri mkubwa wa vitamini.

Inaelezwa kwamba, kutokana na uzuri wa tunda hili, mvumbuzi maarufu anayeaminika kulivumbua Bara la Amerika, Christopher Columbus, alilipachika papai jina la ‘Tunda la Malaika’.

Mbegu za papai huliwa pia, ingawa zina ladha chungu, lakini hazina madhara bali zina faida kiafya.

Tunda na mbegu zina aina pekee ya kimeng’enyo (enzymes) kiitwacho Papain, ambacho ni muhimu katika kusaidia usagaji wa protini mwilini pia hutumika kama dawa mwilini ya kutibu majeraha kwenye utumbo na matatizo mengine.

Kimeng’enyo hicho hupatikana kwa wingi pale papai linapokuwa bado bichi. Kwa kawaida mapapai mabichi lakini

yaliyokwisha komaa vizuri, ndiyo hutumika kupata virutubisho hivyo ambavyo hutengenezwa vidonge vya lishe (Food Suplements).

Papai ni chanzo kikuu cha virutubisho vinavyotoa kinga kubwa ya mwili (antioxidants) kama vile Carotenes, Vitamini C, Flavonoids na jamii zote za Vitamin B. Mbali ya kuwa na Vitamini, papai pia lina madini ya Potassium, Magnesium na Fiber.

Virutubisho vyote hivyo vina kazi kubwa mwilini ya kuimarisha utendaji kazi mzuri wa mfumo mzima wa moyo na kutoa kinga kubwa dhidi ya ugonjwa wa saratani ya utumbo. Hivyo ulaji wa tunda hili, ni tiketi ya uhakika ya kwenda mbali na matatizo ya moyo na saratani ya utumbo.

Vile vile papai linaweza kuwa na msaada mkubwa katika kuzuia kisukari kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha vitamini C, E na A, vitamani ambazo zina nguvu na ni muhimu sana katika kutoa kinga dhidi ya magonjwa hayo. Vitamini hizo pia ndizo zinazozuia  ile hali ya kuganda mwilini kwa mafuta aina ya Cholestrol (Oxidation of Cholestrol).

Cholestrol inapoganda, ndipo inapokuwa na uwezo wa kukwama na kujikusanya kwenye kuta za mishipa ya damu na kuanza kutengeneza uzio hatari ambao husababisha mshituko wa moyo au kiharusi.

Njia pekee ya kupambana na hali hiyo isitokee mwilini mwako ni kula kwa wingi papai lenye kiwango kikubwa cha vitamin E na C ambazo ndizo zinazodhibiti kuganda kwa mafuta mabaya na mazuri ya Cholestrol.

Papai pia lina kirutubisho kingine muhimu aina ya Fiber (ufumwele) ambacho kimeonesha uwezo mkubwa wa kushusha kiwango cha Cholestrol mwilini.

Umuhimu wa kirutubisho aina ya Fiber, kilichomo kwenye papai, ni mkubwa kama vile kusaidia usagaji wa chakula tumboni hivyo kumuwezesha mtu kupata choo laini, na kirutusho hiki kimeonesha uwezo wa kutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo ambayo huwa na uhusiano mkubwa wa mtu kukosa choo kwa muda mrefu au kupata kwa tabu.

Virutubisho vyote vilivyomo kwenye papai hutoa kinga ya pamoja kwenye chembe hai za utumbo dhidi ya vijidudu nyemelezi. Hivyo kwa kuongeza ulaji wa tunda hili, unakuwa unajipa kinga madhubuti dhidi ya magonjwa tuliyoyataja hapo juu.


Post a Comment

0 Comments