habari Mpya


Viongozi Watoa Pole baada ya Maduka zaidi ya 600 yateketezwa kwa Moto Mbagala-Dar.

Baadhi ya mabaki ya vibanda vilivyoungua moto Mbagala Rangitatu

Zaidi ya maduka 600 ya wafanyabiashara ndogo yameteketea kwa moto katika Soko la Kamkochea lililopo Mbagala Rangitatu jijini Dar es salaam huku taarifa za awali zikieleza kuwa moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme.

Moto huo uliotokea alfajiri ya March 6, 2018 uliendelea kuwaka hadi majira ya saa 3 asubuhi kwenye baadhi ya maeneo ya soko hilo huku baadhi ya wafanyabiashara wakishindwa kujizuia na kulia  kwa uchungu na wengine kukosa cha kusema wala kufanya baada ya kukuta maduka yao yakiwa yameteketea.
Baadhi ya wananchi wakiwa eneo la tukio ambapo Soko hilo ambalo lilikuwa na wafanya biashara zaidi ya 500.

Licha ya Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika kwenye soko hilokwa wakati , bado lilitupiwa lawama ya kutokuwa na maji ya kutosha kuuzima moto na hivyo wananchi kuamua kufanya jitihada zao binafsi kukabiliana na moto huo.

Akijibu tuhuma mbalimbali zilizotolewa na wananchi kuhusu kushindwa kuzima moto huo kwa wakati, msemaji wa Jeshi la Zimamoto kutoka makao makuu amesema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zilizosababisha hali hiyo.
Vibanda vilivyokuwa vinamilikiwa na wafanyabiashara wa Soko la Mbagala Rangi Tatu vikiwa vimeteketea kwa moto.

Mkuu wa wilaya ya Temeke, Bw.Felix Lyaviva mara baada ya kufika kwenye eneo hilo aliwaomba wananchi hao kuwa na utulivu na kuahidi kuchukua hatua za awali za kuwapatia maeneo mengine ya kufanyia biashara.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri wa Temeke jijini Dar es Salaam, Nassib Mmbagga ametoa pole kwa wafanyabiashara wa soko hilo na  amesema Halmashauri imepanga kukutana na wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika soko hilo.

Amesema lengo ni  kuangalia ni jinsi gani halmashauri itawasaidia.

Post a Comment

0 Comments