habari Mpya


Ngara/Kagera - Kisa cha Mtoto Anthony kuzuia Baba yake Kuuza Shamba.

Na Shaaban Ndyamukama, Radio Kwizera FM-Ngara/Kagera.

Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Ngundusi wilaya ya Ngara mkoani Kagera amemtishia baba yake kumfikisha kituo kidogo cha polisi Kabanga wilayani humo akizuia kuuzwa kwa shamba la familia yao.

 Mwanafunzi huyo Anthony Petro (10) amekuwa jasiri kumzuia baba yake asiuze shamba baada ya kuona akisaini barua ya mauziano na mtu aliyemfahamu akidai anaitwa Misheli, kiongozi wa kanisa katoliki kigango cha Ngundusi kata ya Kabanga wilayani Ngara.

Taarifa za mwanafunzi huyo kupinga uamuzi wa baba yake zilianza kusambaa wiki iliyopita kupitia video ya makundi ya mtandao wa WhatsApp akiibua hoja na hisia ya kutaka kufahamu undani wake kwa kutumia polisi wa Kabanga.
Akizungumza Machi 11,2018 nyumbani kwa baba yake katika kijiji cha Ngundusi kata ya Kabanga, mtoto huyo alisema aliamua kuzuia kuuzwa shamba ili yeye na ndugu zake wawili wa kike wasikose sehemu ya kuishi.

Alisema nyumbani wanaishi maisha ya dhiki na taabu wakitegemea baba yao mzee anayefanya shughuli za kilimo lakini akienda mitaani kuokota chupa za plastiki na kuziuza ili akapate fedha ya chakula.

"Alitaka kuuza shamba ili sisi tukaishi wapi, na tukalime wapi au tutatunzwa na nini?" Alihoji na kuongeza " Nikitoka shuleni nakuja mjini kabanga hadi kobero kutafuta misaada ya hela nikanunue unga wa kula na wadada zangu"

Katika familia ya mtoto huyo iliyo mbali na makazi ya watu, ina maisha duni kwani watoto wanategemea kuokoteleza chupa na madumu ya plastiki na kuwauzia watengenezaji wa pombe za asili wakitembea mpaka mji wa Kobero nchini Burundi kuuza chupa na madumu hayo

Pia mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ngundusi Josia Cleophace alisema mwanafunzi Anthony si mzuri sana kitaaluma kwani mahudhurio yake ni wastani anakuwa akienda kwenye vibanda vya wafanyabiashara kuomba misaada ili kupata chakula cha familia
 

Alisema anasoma darasa la kwanza lakini dada zake wawili wanasoma darasa la pili wakipishana miaka baada ya yeye kuugua muda mrefu na kudumaa na zaidi alisumbuliwa na funza kwa maana baba yake ni mzee hivyo alishindwa kumsaidia kimazingira

Baada ya kugundua hali ya familia tulimchangia Sh15,000 akanunua dawa ya kuoshea mifugo na mafuta ya mgando kisha kupona funza na amekuwa darasa la awali miaka miwili” Alisema Mwalimu Josias

Aliyedaiwa kununua shamba Michael Nazali ( Misheli) amekana kutohusika katika manunuzi ya hivi karibuni ispokuwa mwaka 2000 ndipo alinunua sehemu yenye ukubwa wa hatua 20 kwa 50 na kwamba hujitokeza kumsaidia kutokana na ugumi wa maisha yake na familia

Alipohojiwa maisha yake Mzee Petro Magogwa alisema amekuwa dhaifu baada ya kufiwa na wake zake wawili huku wawili wakiachika kati yao watatu walitoka Burundi ambapo wawili walio hai waliondoka na watoto wake watatu

Pia alisema anao watoto watatu wa kike wameishaolewa na kuzaa wajukuu lakini pia hawakujaliwa kupata familia imara kiuchumi hivyo anapougua au kuuguza msaada wake ni kukata sehemu ya shamba na kuuza huku akitembeza chupa za plastiki

"Watengeneza pombe wananipatia Sh500 kwa chupa 24 wakati mwingine kwa siku napata Sh 2000 nanunua unga wanangu wasilale njaa" Alisema huku akibubujikwa machozi.

Alisema anaishi kwa mara ya mwisho aliuza sehemu ya shamba miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua muda mrefu na watoto wake kwa thamani ya Sh120, 000 na alitumia kununua mahitaji na dawa.
Mzee huyo anao watoto watatu anawalea ambao ni Eliza Petro (9), Editha (13) wote darasa la pili akiwemo Antony na amejaliwa kuoa wanawake wanne na kuzaa watoto 19 lakini tisa walipoteza maisha kwa nyakati tofauti.

Mke wa kwanza walizaa watoto wanane wakafariki watano wa kiume na kubaki watatu wa kike wote waliolewa mmojawapo yupo Burundi aliondoka na mama yake ambapo mke wa pili mtanzania alizaa watoto wanane kati yao saba wakafariki na kabaki mmoja msichana anayeishi wilayani Kahama.

Alisema mke wa watatu naye raia wa Burundi alizaa naye watoto watano na wawili wa kiume walifariki na kubaki watatu wa kike nao baada ya mama yao kufariki walichukuliwa na mama zao wadogo pamoja na wajomba pia wanaishi nchini Burundi

Baada ya mke wa tatu aliyezaa naye watoto wanne wawili wa kiume na wawili wa kike kufariki kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba , mtoto wa kiume alifariki baada ya miezi minane na kubaki na hao waliopo akiwemo huyo Anthony anayetetea ndugu zake akizuia shamba kuuzwa.

Bahati yangu mbaya na watoto wa kiume miaka miwili ilipita nilioa mke mwingine wa nne na kuzaa naye mtoto mmoja wa kiume, mtoto huyo alifariki na mama yake kuondoka na kubaki na hawa mnaowaona ila sina nguvu za kuwatunza” Alisema Petro Magogwa

Mkuu wa kituo cha polisi Kabanga wilayani Ngara Benadi Masakia amekiri kupokea taarifa za Anthony kuzuia baba yake kuuza shamba pia ameshirikiana na askari wenzake wa polisi jamii kumsaidia mzee Petro Sh 35,000 ili akawanunulie chakula na sabuni watoto wake.


Post a Comment

0 Comments