habari Mpya


Kanisa la Adventist la Wasabato Lasaidia Watoto wa Kituo cha Nazaleti wilayani Ngara.

Vijana wa Kanisa la Adventist la Wasabato wilayani Ngara mkoani Kagera limefanya ibada ya wiki katika kituo cha kulelea watoto Yatima na Waishio  Mazingira magumu cha Nazaleti wilayani humo kisha kutoa msaada wa vitu mbalimbali  vyenye thamani ya Sh 500,000.

Msaada wa vitu hivyo  ni  sabuni, mchele, mafuta ya kupikia ,nguo, madaftari sukari na kalamu ambapo  vimekabidhiwa na vijana watafuta njia wa kanisa hilo  kwa kuwaona  wenzao wanaolelewa katika kituo cha Nazaleti wilayani hapa.
 
Akitoa mahubiri ya neno la Mungu  Mzee wa kanisa hilo Maila Mugeta alisema, mkono wa Mungu  uendelee kuwabariki na kuwatia baraka  wasimamizi wanaolea watoto hao, wakijaliwa moyo wa huruma, kufundisha upendo na imani za kiroho.

Mugeta alisema watoto hao wanahitaji  chakula na huduma nyinginezo wakati wakifundishwa elimu ya dunia kupata ujuzi wa kitaaluma kupitia fani mbalimbali, wakielekezwa kumfuata kristu kufundishwa maadili mema mbele za Mungu. 

Aidha mkuu wa kituo cha Nazaleti wilayani Ngara Francisca Bazimenyela amesema watoto wanaolelewa kituoni hapo wanafikia 30 kati yao wapo waliofiwa na Wazazi na wengine kutelekezwa kutokana na migogoro ya ndoa na kifamilia.

“Watoto hawa walikosa malezi na elimu hivyo tunawapatia maadili ya kijamii na kiroho changamoto kubwa ni kupungua wafadhili na hatuna shamba la kutuwzesha kulima mazao ya chakula na  bustani ya mbogamboga”.Alisema Francisca.
 

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo Masumbuko Bwire amesema kanisa la Sabato Ngara mjini pia limetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wafungwa wa gereza la Ngara ikiwa ni utekelezaji wa wiki ya huruma  kumuenzi Kristu aliyefia msalabani

Bwire alisema katika kipindi hiki cha Kwaresma waumini wanatafakari mafundisho ya Kristo wakati alipokuwa akiwataja watu wenye shida na kuwahudumia kama walemavu, wasioona na watoto waliomkimbila.

Pia waumini hao wametembelea Hospitali ya Nyamiaga wilayani Ngara kutoa msaada wa damu kwa ajili ya wagonjwa hasa watoto wachanga, wajawazito wanaojifungua kwa upasuaji na wanaopata ajali za matukio mbalimbali.
 

Post a Comment

0 Comments