habari Mpya


Tido Mhando Afikishwa Mahakamani kwa Kosa la matumizi Mabaya ya Madaraka.

tido-1
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), Tido Mhando (kushoto), akiwa mahakamani na watuhumiwa wenzake. 
 
 Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), Tido Mhando, amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar leo January 26,2018 kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa TBC.
 
Tido ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media anakabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya matumizi mabaya ya madaraka ambapo moja ya mashtaka hayo ni uhujumu uchumi na kuisababishia TBC hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 887.
 

Katika kesi hiyo, Tido amesomewa makosa yake na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)Leornad Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
 
Swai amedai Tido anakabiliwa na makosa matano ya uhujumu uchumi na kuisababishia TBC hasara, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ametoa kibali cha kesi hiyo kusikilizwe mahakamani hapo.
 
Katika kosa la kwanza ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka, Tiido anadaiwa June 16,2008 akiwa Dubai kama mtumishi wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya uendeshaji wa vipindi kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BVI) bila ya kutangaza zabuni na kuinufaisha channel hiyo.
 
Kosa la pili, anadaiwa June 20, 2008 akiwa huko huko Dubai kama Mkurugenzi Mkuu wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya kiutendaji kati ya TBC na Channel 2 bila kutangaza zabuni.
 
Kosa la tatu, anadaiwa kati ya August 11,2008 na September 2008 akiwa Dubai kama mwajiriwa wa TBC kwa makusudi alisaini mikataba ya kununua, kusambaza na kusimika vifaa vya kurushia matangazo kati ya TBC na Channel 2 bila kutangaza zabuni ya manunuzi na na kuinufaisha channel hiyo.
 
Kosa la nne, anadaiwa alilitenda November 16, 2008 akiwa Dubai kwa makusudi alisaini mikataba ya uendeshaji wa miundombinu ya DTT kati ya TBC na Channel 2 bila kutangaza zabuni ambapo aliinufaisha channeli.
 
Kosa la tano, anadaiwa kati ya June 16 na November 16,2008 akiwa Falme za Kiarabu, kama mwajiriwa wa TBC kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu kwa mamlaka yake alilisababishia shirika la TBC hasara ya Sh.Mil 887,112,219.19.
tido-2
Tido aliyakana mashtaka yote ambapo Wakili Swai alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika  na wakili wake Ramadhan Maleta, Tido aliiomba Mahakama hiyo impatie dhamana ambapo Hakimu Nongwa alitoa masharti ya kumtaka Tido atoe fedha taslimu Sh.Mil 444 ama mali isiyohamishika ya thamani hiyo, kuwa na wadhamini wawili ambapo kila mmoja asaini bondi ya Sh. milioni 500 na hatakiwi kutoka nje ya nchi bila kibali cha Mahakama.
 
Tido ametimiza masharti hayo na kutoa hati ya mali yenye thamani ya Sh.Mil 444 pamoja na kuwa na wadhamini ambapo kesi imeahirishwa hadi February 23,2018.
 
TUJIKUMBUSHE.
 
Tido alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC kati ya mwaka 2006 na 2010. Awali alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la BBC (1999-2006).
 
Kwa kipindi cha miaka mingi alikuwa akifanya kazi ya utangazaji wa radio ambapo alianza Utangazaji mwaka 1969 akiwa Radio Tanzania Dar es Salaam, (RTD), baadaye akafanya kazi Kenya, halafu Uingereza na hatimaye akarejea tena RTD kabla ya kuwa TBC.
 
Kwa sasa Tido Muhando ni Mkurugenzi Mkuu wa Azam Media.
 
Chanzo- /globalpublishers.

Post a Comment

0 Comments