habari Mpya


Askofu Jacob Chimeledya - Viongozi toeni Huduma kwa Moyo wa Huruma na Upendo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la  Anglican Tanzania, Jacob Chimeledya akimvika Msalaba wa Kiaskofu , Askofu Darlington Bendankeha  wakati wa ibada ya Kusimikwa kwake kuwa Askofu Mkuu Kanisa la Anglican Dayosisi ya Kagera,mkoani Kagera leo October 29,2017  katika Kanisa Kuu la Murgwanza wilayani Ngara mkoani Kagera.
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la  Anglican Tanzania, Jacob Chimeledya -Pichani kulia, amewataka Viongozi wa wanaotoa huduma za kiroho pamoja na Watendaji wa Serikali kutoa huduma kwa  Jamii kwa  kutanguliza moyo wa huruma na upendo katika kujenga misingi ya heshima na utawala bora.

Askofu Chimeledya ametoa wito huo hii leo (Oktoba 29,2017) wakati wa ibada ya kumsimika Askofu wa nne wa Anglican Dayosisi ya Kagera iliyoanzishwa mwaka 1985 kutoka dayosisi ya Viktoria Nyanza -Mwanza

Amesema kila kiongozi wa kiroho anafananishwa na Nabii Petro wakati akichunga kondoo wa mungu ambao ni waumini chini ya usimamizi wa Yesu hivyo wachungaji na maaskofu wasitangulize tamaa, uchonganishi na wawe wavumilivu katika kuongoza waumini wao

Akitoa mahubiri katika ibada hiyo amemtaka askofu Bendankeha kufuata mafundisho na maelekizo ya kanisa anglikana wakiwemo hata wapinzani wake ambao waliunda vikundi vya kupinga kusimikwa kwake kuongoza dayosisi hiyo
Aidha amesema katika kuongoza kanisa na dayosisi hiyo ahakikishe anatoa mchango wa kukemea vitendo vya unyanyasaji wa  watoto ambapo kwa sasa vitendo hivyo ni 38% hapa Tanzania

Alisema kila kanisa nchini watoto wanne kati ya 100 wanakumbwa na kadhia ya unyanyasaji na ukatili kuanzia ngazi ya familia na kwenye jamii hivyo kanisa kwa kushirikiana na vyombo vya dola ni kuungana kupinga pia kutokomeza vitendo hivyo

"Watoto wanayo haki ya kuishi kupata huduma za kijamii zikiwemo za kiroho kuwajengea misingi ya kupata malezi na maadili mema yanaorandana na tamaduni za  kitaifa" alisema Chimeledya

Pia alisisitiza kujihadhali na ubaguzi wa kikabila katika utoaji wa huduma bali uongozi wa aina yoyote uzingatie misingi ya baba wa Taifa Hayati mwalimu Julius Nyerere ya umoja wa kitaifa kwa makabila yote kutambuana kama taifa moja na kiimani yote yako chini ya Mungu.
Kwenye ibada hiyo,Waziri wa Katiba na Sheria  wa Tanzania Prof.Palamagamba Kabudi amewataka Maaskofu wa Kanisa la Anglican nchini kutumikia waumini kama mashemasi badala ya kuibua migogoro ya kugombania nafasi ya uaskofu na kusababisha uvunjifu wa Amani, kiroho na kijamii.

Alisema katika kutumikia nafasi ya kuwa askofu lazima kuzingatia miito ya mungu na Kristo kwani kikatiba imeandikwa kila atimizaye miaka 65 anapaswa kumpisha viongozi mwingine hivyo askofu mteule atumie kipaji taaluma na karama zake kuwsunganisha waumini na kanisa ili kumtumikia mungu na waliomuweka katika daraja alilopewa

Alisema serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini likiwemo kanisa la Anglican nchini katika utoaji wa huduma za kiroho lakini na huduma nyinginezo za kijamii na kwamba serikali hiyo hiyo inatafuta fursa za kupata fedha kuboresha miundombinu katika mazingira ya wananchi mikoa yote nchini

Pia Waziri Kabudi alisema mojawapo ya miradi mikubwa inayohitajo fedha kupitia mapato ya ndani kujenga reli inayokwenda kupitia wilaya ya Ngara kuelekea nchi za Rwanda na Burundi huku pia kujenga bwawa la umeme wamegawati 2100 ili kuwezesha hata kuchimba madini ya nickel wilayani humo na kisha kuanzisha viwanda ili kuongeza ajira nchini.

Naye askofu mteule Darlington Bendankeha ameitaka serikali kuwalinda watanzania kwa kuimarisha ulinzi na usalama kutokana na matukio ya uvunjifu wa amani  ambayo kwa sasa inaonekana kulegalega baada ya tukio kubwa la hivi karibu la kujaribu kuuawa Tundu Lisu ambaye alijeruhiwa na kufifiza juhudi zake za kuwasemea wananchi kukemea baadhi ya matendo ya ubadhilifu wa rasilimali za nchi.
 
Pia alisema Rais katika utendaji wake na washauri alio nao kufikiria suala la kufufua mchakato wa katiba mpya ambayo ni kiu kubwa ya watanzania kukuza demokrasia, haki za binadamu  na utawala bora ambayo katika kuleta maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa.

Katika hatua nyingine,Askofu Chimeledya alitumia nafasi yake kuipongeza serikali chini ya Rais Magufuli kudhibiti ubadhilifu wa rasilimali za taifa ikiwemo rasilimali madini hivyo usimamizi na mapato yasaidie kuboresha miundombinu ya kijamii kama maji afya barabara, elimu na ujenzi wa reli nchini

Aliwataka watendaji wa serikali na wanasiasa kufanya kazi kwa uadilifu badala ya kubeza juhudi za Rais anazofanya na kufanya ubadhilifu kwa kuonesha uchungu na nchi yake katika kuongeza mapato kiuchumi na hatimaye kuondoa umaskini na kujipatia maendeleo.

Alisema seikali iwe na matumizi bora ya fedha zitokanazo na rasilimali kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato na kwamba kanisa la Anglican linaungana na juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli  katika kuwakwamua wananchi kiuchumi akilenga kuondoa umaskini.

Habari/Picha Na-Shaaban Ndyamukama.

Post a Comment

0 Comments