habari Mpya


REKODI NYINGINE: Bibi Atimiza Miaka 110 Akiwa Duniani, Ngara-Kagera.

Alizaliwa mwaka 1910, na leo February 4,2020 ametimiza miaka 110 akiwa duniani. 

Habari /Picha Na Auleria Gabriel /  Bob Maurice -RK Ngara.
 Ni Bi. Vanis Barahaza mkazi wa kitongoji cha Mukidyama kata ya Ngara mjini wilayani Ngara mkoani Kagera ambaye aliolewa mwaka 1941 kwa Bw. George Barahaza Nakumuhana na kujaliwa kupata watoto saba.

Kati ya watoto hao, watano walikwishafariki na kubaki na watoto wawili lakini pia mumewe Bw. George alifariki mnamo mwaka 1979 hivyo ameishi naye kwa miaka 38 pekee.

Kwa sasa bibi huyu kwa sasa hana uwezo wa kusikia vizuri wala kutembea, lakini anaona, anaongea na anaonekana kuwa mwenye afya njema.

Redio Kwizera mapema leo,February 4,2020 asubuhi imefika nyumbani kwa Bi. Vanis na kukuta shamra shamra zikiendelea za kumuandalia sherehe ya kufikia siku yake ya kuzaliwa. 
Bi. Dorothea Barahaza ni mtoto wa mwisho wa bibi huyu ambaye naye kwa sasa ana miaka 60 na ndiye anamtunza mama yake. Anasema, mama yake hakufanikiwa kusoma lakini shughuli yake kuu ilikuwa ni ukulima na usukaji wa mikeka.

Ninachojivunia ni kuona kwamba mama anampenda Yesu, na ndio maana Mungu anaendelea kumlinda na kumtunza. Akiwa amelala unaweza kusikia akiomba kwa lugha ya Kihangaza, yani ninajivuna kabisa kwamba yumo ndani ya Yesu.” Alisema Bi. Dorothea.

Mpaka sasa bibi huyu ana wajukuu 15 na vitukuu 40 ambao wapo kwenye mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

Baadhi ya majirani wa bibi huyu wamesema ni jambo la kujivunia kuona wanaishi na mzee ambaye ameweka historia ya kuishi miaka mingi kwani wamejifunza mambo mengi kutoka kwake.

Najionea fahari sana kuwa na bibi yetu huyu, kwa sababu ni miongoni mwa watu wachache na ni ishara ya kuonesha kwamba maisha ya kujituma na kufanya kazi na kula vizuri vyakula vya asili vimechangia kwa sehemu kubwa kuwa na umri mkubwa.”Anasema Bw. Absalum Nvyankende ambaye ni mchungaji katika kanisa la Anglikana-Murgwanza wilayani Ngara.

Bibi huyu huenda akawa miongoni mwa wazee wakongwe zaidi nchini Tanzania anayepatikana na pia ameweka rekodi ya kuwa na miaka mingi duniani.

Historia inaonesha kuwa Japan inatajwa kama nchi yenye kusifika kuwa na watu wenye umri mkubwa zaidi duniani kwa kuwa watu wengi huishi zaidi ya miaka 65. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Mawasiliano nchini Japan, kufikia mwezi Februari 2018, watu 69,000 wameishi zaidi ya miaka 100.

Je, Tanzania ina utaratibu wa kufuatilia maisha ya wazee walioishi umri mrefu zaidi duniani? Bi. Vanis anaweza sasa kuanza kuamsha ari hiyo.

Post a Comment

0 Comments