habari Mpya


Miili ya Watu 20 waliofariki Kongamano la Mwamposa Kuagwa Leo.

Uwanja wa majengo, Moshi mkoani Kilimanjaro unavyoonekana baada ya ibada ya jana iliyoongozwa na Mtume Boniface Mwamposa kugeuka vilio baada ya watu 20 kufariki dunia walipo kanyagana wakipita kwenye ‘mafuta ya upako’.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amesema miili ya watu 20 waliofariki kwenye kongamano la Mtume na Nabii Mwamposa, inaagwa leo Februari 3, 2020, kwenye viwanja vya Majengo mjini Moshi. 

Amesema hadi sasa tayari miili 16 imeshatambuliwa.


Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ,IGP Simon Sirro amewataka Watanzania kuwa  makini kwani kinyume na hapo itakuwa shida sana na kuongeza iko haja kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa kuanza kuyafuatilia makanisa yote nchini na hasa makanisa madogo madogo ambayo sasa yamekuwepo kila mahali.

"Sio kila padri, mchungaji basi anataka kuwachunga kondoo wake waende kuuona ufalme wa Mungu, wengine wanahangaika na utafutaji tu wa maisha.Sio kwamba nahukumu lakini kuna mambo ya kujifunza,"amesema

Kuhusu Polisi iwapo walikuwepo kwenye kongamano hilo la Mwamposa, IGP Sirro amesema ameshatoa maagizo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimajaro kufuatilia na iwapo walikuwepo polisi lazima waulizwe imekuaje hadi watu wakapoteza maisha na wao wakiwepo, kwani sheria lazima ichukue mkondo wake.

Nae Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema wamemkamata Mtume Boniface Mwamposa Jijini Dar es salaam alipokuwa amekimbilia baada ya kutoroka mkoani Kilimanjaro kutokana na tukio la waumini wake kugombea kukanyaga mafuta ya upako na kusababisha vifo vya watu 20.

Kutokea kwa tukio hilo,amesema Wizara itaweka Kanuni na Taratibu kali za Usajili wa Taasisi zinazotoa Huduma za Maombezi(Ministries) ambazo baadhi zinavunja Sheria.

Post a Comment

0 Comments