habari Mpya


ASKOFU NIWEMUGIZI: Vifo vilivyotokea Moshi kutokana na watu kugombania mafuta ni upuuzi.

HABARI NA Opiyo Vincent
PICHA NA Bob Maurice
Askofu wa jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi amekikashifu kitendo kilichotokea mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wiki iliyopita cha watu 20 waliofariki na wengine wengi kujeruhiwa baada ya kukanyagana waking’ang’ania mafuta ya upako.Askofu Niwemugizi amewatahadharisha waumini kuhusu manabii wa uongo wanaotumia jina la uchungaji kuwalaghai na badala yake wamuombe mwenyezi Mungu awaepushe na udanganyifu unaotokea kwa kutumia mambo ya kiimani.

“Wale watu wamekufa ni kwa sababu ya ujanja wa watu wanaotumia jina la uchungaji vibaya, watu wanaojiita manabii sijui mitume lakini kwa kweli ni watafuta pesa tu, ni upuzi,” alisema baba Askofu.

Askofu Niwemugizi amezungumza haya katika mahojiano ya kipekee na Radio Kwizera FM baada ya kuongoza ibaada ya misa takatifu katika kanisa la mtakatifu Francisko wa Assisi parokia ya Ngara mjini Jumapili ya Februari 09, 2020.

“Hata mtu mwenye akili akiskia mambo ya kinabii anaamini kwamba huyu anayezungumza kweli ametumwa na Mungu lakini tujue kwamba Mungu amesema watatokea watu wengi watakaojifanya wao ni wakristu na watadanganya wengi na hayo ndio matokeo ya watu wanaotumia jina la Mungu vibaya.”

“Sisi tumetumia vitu hivi; mafuta matakatifu, chumvi, maji kwa zaidi ya miaka elfu mbili lakini kitu kama hiki hakijawahi kutokea. Watu wanadanganyika, watumie akili pia kuepukana na hao wajanja wanaolifanya taifa kuingia katika mtafaruku mkubwa sana,” alisema Askofu Niwemugizi.

Baba askofu amezungumzia pia umuhimu wa kupanga maombi ya pamoja na madhehebu mengine wilayani Ngara mkoani Kagera ili kumuomba mwenyezi Mungu kuwaepusha na ulaghai unaojitokeza katika jamii na kuleta msononeko ambao haufai kuwepo.

Mhashamu Severine Niwemugizi, ameyasema haya ikiwa ni siku moja tu baada ya kuwasili jimboni akitokea Roma nchini Italiaa kuhudhuria mkutano wa maaskofu kote ulimwenguni.


Post a Comment

0 Comments