habari Mpya


AJALI MBAYA WILAYANI NGARA: Watatu wafariki papo hapo na zaidi ya 30 wajeruhiwa.

HABARI NAAuleria Gabriel
PICHA NA: Godfrey Bisambi 
Watu watatu wamefariki papo hapo na wengine zaidi ya 30 wamejeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya magari matatu kwenye mteremko wa K9 kijiji cha Kasharazi wilayani Ngara mkoani Kagera.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa sita mchana ikihusisha gari la abiria aina ya TATA Kampuni ya Matunda iliyokuwa iktokea wilayani Kahama, gari dogo la NOAH mali ya Sialeo Ernest mkazi Ngara ikitokea Benaco na Lori aina ya Scania iliyokuwa ikielekea Nchini Burundi.
Akiwa katika eneo la tukio, Mkuu wa jeshi la polisi wilayani Ngara Abeid Maige ameiambia Redio Kwizera kwamba watu hao waliofariki papo hapo ni mwanamke, mwanaume na mtoto na majeruhi wamepelekwa katika hospitali za Nyamiaga na Murgwanza zilizopo wilayani Humo.
 “Inaonekana ni ‘speed’ za madereva ndizo zimesababisha ajali kutokea, lakini mpaka sasa hivi kuwa watu wazima wawili wamefariki pamoja na mtoto mdogo na majeruhi wote tumeshafanya jitihada za kuwapeleka hospitali za Nyamiaga na Murgwanza, kwa hiyo matibabu yanaendelea kule. Kwa hiyo taarifa kamili zaidi zitatolewa na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kagera RPC Revocaus Malimi” Alisema OCD Maige


Akizungumzia majeruhi waliopokelewa katika hospitali za Nyamiaga na Murgwanza, Mganga mkuu wa wilaya ya Ngara Dr. Revocatus Ndyekobora amesema wamepokea majeruhi 34 na baadhi yao hali zao sio nzuri.
“Jumla ya majeruhi tuliowapokea ni 34, Nyamiaga wamepokea majeruhi 9 na Murgwanza wapo majeruhi 25. Katika hao Majeruhi, Nyamiaga majeruhi wawili hali zao sio nzuri na hapa Murgwanza majeruhi watano hali zao sio nzuri.”
Bado tunaendelea na huduma ya kwanza kwa majeruhi wote baadaye ndio tutajua ni majeruhi wangapi tutakaowapa rufaa na wangapi tutakaoendelea nao.” Alisema DMO Ndyekobora


K9 ni barabara kuu iendayo Burundi na ni eneo lenye mteremko mkali ambapo mara nyingi kumekuwa kukishuhudiwa ajali mbaya ingawa kuna vibao vinavyotoa tahadhari kwa watumiaji wa vyombo vya moto kupunguza mwendo wanapofika katika eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments