habari Mpya


Mawaziri wa Nishati Burundi, Rwanda na Tanzania Wagoma Kuongeza Muda Mradi wa Umeme Rusumo.

Pichani ni mawaziri wa Nishati kutoka Tanzania ,Rwanda na Burundi pamoja na wasimamizi wa mradi wakiwa eneo la mradi wa Umeme
NGARA NA MWANDISHI WETU AULERIA GABRIEL/PICHA NA LAMECK .
Serikali za Tanzania, Burundi na Rwanda zimesema hazitakubali kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kufua Umeme wa maji unaotekelezwa na nchi hizo kupitia maporomoko ya mto Kagera katika kijiji cha Rusumo wilayani Ngara mkoani Kagera na wilaya ya Kirehe nchini Rwanda.


Tamko hilo limetolewa na waziri wa Nishati wa Tanzania Dr. Medard Kalemani wakati wa kikao baina ya mawaziri watatu wa Nishati kutoka nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania waliokutana hii leo Disemba 06,2019 kukagua maendeleo ya mradi huo.
Pichani ni moja ya eneo la mradi wa Umeme
Kupitia mkutano huo baina ya Waziri wa Nishati wa Tanzania Dr. Medard Kalemani, Waziri wa Miundombinu wa Rwanda Claver Gatete na waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi Mhandisi Come Manirakiza, mwenyekiti wa mawaziri hao Dr. Medard Kalemani amesema, wamepokea maombi ya kuongezwa muda wa ukamilishaji lakini baada ya kujadiliana wameona haiwezekani kuendelea kutoa muda wa ziada kwani kazi itachelewa.
“Tumemtaka mkandarasi pamoja na wasimamizi, wakamilishe kazi ndani ya muda. Na muda uliotarajiwa kukamilika kwa kazi zote na mradi kuanza kufanya kazi ni mwaka 2020”
“Huu umeme tunauhitaji sana watanzania na wenzetu wa Rwanda na Burundi, ndio mana tumetaka mradi ukamilike haraka. Alisema Dr. KalemaniMradi wa ujenzi wa kufua umeme wa maji wa Rusumo, ulisainiwa tangu Februari13, 2017 na unatakiwa kukamilika Februari mwaka 2020, lakini huenda isiwe kama ilivyokusudiwa kutokana na mkandarasi kuendelea kuomba muda usogezwe mbele.
Mpaka sasa mradi huo wenye Megawatt 80 ambapo kila nchi itapata Megawatt 27, umefikia asilimia 59 na unagharamiwa na nchi washirika kupitia wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Maendeleo Afrika (AfdB) na Benki ya Dunia (WB) ambapo kwa kuzalisha umeme kila nchi inachangia takriban Dola za Marekani milioni 113 na kwa upande wa njia ya kusafirisha umeme kila nchi inachangia Dola za Marekani milioni 36.7

Mkutano huu wa Disemba 06, 2019 ndio wa mwisho kwa waziri Dr, Kalemani kuuongoza na tayari amekabdhi nafasi hiyo ya uwenyekiti kwa waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi Mhandisi Come Manirakiza ambaye ataanza kuongoza kwenye mkutano ujao utakaofanyika baada ya miezi sita kuanzia sasa.

Post a Comment

0 Comments