habari Mpya


Mkandarasi wa Barabara Bukoba Apigwa Stop Kutotoka Nje ya Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ametembelea na kukagua mradi wa barabara wa kilometa tano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kujengwa katika Manispaa ya Bukoba mkoani humo,wenye thamani ya shilingi bilioni 7.3 ambapo hakuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya JASCO Building and Civil Engineering Contractors ya Jijini Mwanza.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alimweleza Mkandarasi huyo kuwa mradi unasuasua na asilimia ya ujenzi ni 40 tu wakati alitakiwa awe amevuka hapo ambapo alimwagiza kutotoka nje ya mkoa hadi atakapohakikisha kuwa mradi huo unaendlea vizuri. 

Aidha, alimweleza mkandarasi huyo kuhakikisha fedha anazolipwa na Manispaa ya Bukoba kutekeleza mradi wa Bukoba na siyo kuhamisha fedha kwenda kutekeleza miradi aliyonayo katika mikoa mingine. 
Nilikuwa nimezuia malipo yako kwasababu nimefuatilia na kugundua kuwa ukilipwa fedha hapa unapeleka kwingine kumalizia miradi ya sehemu nyingine sasa fedha za mradi huu zitalipwa kwenye akaunti ya Bukoba na nitaviagiza vyombo vyangu kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi ya Bukoba na si vinginevyo.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Mwisho Mhe. Gaguti alimweza Mkandarasi huyo wa Kampuni ya JASCO kuhakikisha anawalipa wafanyakazi wake na pasiwepo mtu yeyote anayemdai wakati Manispaa ya Bukoba inamlipa fedha za kutekeleza mradi huo kwa wakati. 

Akimalizia ziara yake Mhe. Gaguti aliwaeleza watendaji hasa wanaopewa jukumu la kusimamia miradi wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa uzalendo kwani Serikali imetoa fedha zote ili miradi ikamilike kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments