habari Mpya


Soma Taarifa ya Habari Saa 24 October 25,2019 Radio Kwizera FM.

Meli ya Mv Victoria Itakapokamilika March 2020.
Source; RK: Ak (polisi)
ED: AG
Date: Friday, October 25, 2019

BUKOBA
Watu 9 wakazi wa mkoa wa Kagera wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za uhalifu kwenye matukio mbalimbali ikiwemo la wizi wa pikipiki.

Akizungumza na vyombo vya habari kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema kuwa kati ya Octoba 11 hadi 22 mwaka huu, umezuka wizi wa pikipiki ambapo zaidi ya matukio 14 yameripotiwa na jumla ya pikipiki 4 zimekamatwa na watuhumiwa wawili wanaohusika na wizi huo.

Amesema kuwa kupitia kampeni maalum ya kuwasaka wahalifu hao jeshi hilo limebaini uwepo wa wimbi la uporaji wa Ng’ombe ambapo jumla ya Ng’ombe 20 wameripotiwa kuibiwa na kati yao, Ng’ombe 7 wameokolewa.

Kwa upande wao baadhi ya waendesha pikipiki za abiria katika manispaa ya Bukoba wamesema kuwa ipo haja ya Jeshi la Polisi kuanzisha ulizi shirikishi ili kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa na kuwakamata wahusika.


Source; RK: Amos J (Ubovu wa Shule) 
ED: AG
Date: Friday, October 25, 2019

SHINYANGA
Zaidi ya Shilingi milioni 40 zinahitajika kwa ajili ya kukarabati na kuboresha miundo mbinu ya shule ya msingi Mwadui C wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kutokana na miundo mbinu ya shule hiyo kuchakaa na kupelekea madarasa kuvuja wakati wa mvua

Wakizungumza na Redio Kwizera, baadhi ya Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wameeleza kuwa wako hatarini kushuka kitaaluma kutokana na uchakavu wa miundombinu ya shule hiyo maana walimu hulazimika kukatisha vipindi na kukimbia maofsini pindi mvua zinaponyesha wakiwa madarasani

Aidha wanafunzi hao wameiomba serikali pamoja na wawadau wamaendeleo kuchangia vifaa kwa ajili ya kukarabati miundombinu.

Katika kutatua changamoto hizo, Benki ya NMB wilaya ya Kishapu imetoa mabati 185 yenye thamani ya shilingi milioni 5 katika shule hiyo pamoja na mbao na mabati 108 yenye thamani ya milioni 5 katika shule ya sekondari Idukilo.


Source; RK: Asma K (Marali)
ED: AG
Date: Friday, October 25, 2019
KAKONKO
Jumla ya kaya elfu 42 katika wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma zinatarajiwa kunyunyuziwa dawa ya ukoko kwa ajili ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa Maralia


Akizungumza na Redio Kwizera, Mganga Mkuu wa Halimashauri ya wilaya ya Kakonko Dr. Joseph Malima Edward amesema maambukizi ya ugomjwa huo katika halimashauri hiyo yapo juu kwa asilimia ni 30.8 ukilinganisha na takwimu za kitaifa

Aidha Dr.Josefu amesema kupitia wizara, wadau mbalimbali na watoa huduma wa afya katika wilaya hiyo wamejipanga kufanikisha zoezi hilo na kwamba watahakikisha wananchi wanakuwa salama bila ya kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo

Hata hivyo amewataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano katika zoezi hilo lakini pia kuendelea kutumia vyandarua kwa ufasaha ili kuhakikisha wanazuia na kutokomza kabisa maambukizi ya ugonjwa wa Maralia


Source; RK: wm (lishe)
ED: AG
Date: Friday, October 25, 2019
BIHARAMULO
Kati ya watoto elfu 4 na 20 waliozaliwa kwenye hospitali, vituo vya afya  na zahanati wilayani Biharamulo Mkoani Kagera katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu,  watoto 217 wamezaliwa wakiwa na uzito pungufu  ikiwa ni sehemu ya viashilia vya udumavu unatokana na lishe duni  kwa mama wajawazito.

Hayo yamebainishwa na mratibu wa Lishe wilaya ya Biharamulo Bw. Salim Idd wakati wa kikao cha kamati ya lishe cha wilaya kinachoketi kila baada ya miezi mitatu kikilenga kufanya tathimini ya hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano na kuendelea.
Amesema watoto wenye udumavu waliobainika katika kipindi hicho walikuwa 141 huku watoto waliobainika kuwa na afya hafifu ni 231 kati ya walengwa elfu 18na 25 na kwamba kamati za lishe za vijiji zinatakiwa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa jamii.

Mwenyekiti wa kikao hicho Bw. Gerald Kilenga amesema maafisa afya na maafisa kilimo kila kijiji wanatakiwa kutimiza wajibu wao wa kutoa elimu ya lishe kwa wanaume na wanawake ili kuondokana na adhari za watoto na mama wajawazito kuzaa watoto wenye uzito pungufu.

Source; Mpekuzi: AG [Ushirikiano]
ED: AG
Date: Friday, October 25, 2019
DODOMA
Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuliunga mkono Shirika la umoja wa Mataifa UN, katika jitihada zake za kuleta maendeleo hapa nchini, kupitia mashirika yake mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, wakati wa sherehe za Shirika la umoja wa Mataifa, katika kutimiza miaka 74 tangu kuanzishwa kwake.

Prof. Kabudi amesema serikali wataendelea kuliunga mkono Shirika hilo kwa juhudi zake, na kwamba wameweka misingi katika Mataifa mbalimbali kupitia mashirika yake, ikiwamo kukuza amani miongoni mwa nchi ikiwemo Tanzania.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa Jackrine Mahon, ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuendelea kupokea wakimbizi na kuwahifadhi, na wanatambua changamoto wanazokutana nazo katika kuwahifadhi wakimbizi na UN wataendelea kushirikiana katika hilo.

Sherehe hizo za Shirika la umoja wa Mataifa, katika kutimiza miaka 74 zilibebwa na kauli mbiu isemayo, ‘wanawake na wasichana wapewe kipaumbele katika kufikia malengo’, na UN lilianza na nchi 51, na mpaka Sasa zimefikia nchi 193 kote ulimwenguni.


Source; Mpekuzi: AG (Agizo)
ED: AG
Date: Friday, October 25, 2019
MTWARA
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara kuwakamata Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wanaotuhumiwa kukimbia na Shilingi Bilioni 1.2 za wakulima ambazo ni madeni ya Korosho.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Newara katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Viwanja vya Stendi Kuu baada ya kupokea Ripoti ya Jumla ya Madeni wanayodai wakulima katika Wilaya za Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newara na Tandahimba.

Baada ya kupokea ripoti ya madeni kwa Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara, Naibu Waziri Masauni amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wengine katika wilaya zilizobakia za Mtwara, Newara, Masasi, Nanyumbu na Tandahimba ambazo katika taarifa ya jumla ya mkoa inaonyesha takribani Shilingi Bilioni 1.2 bado zinadaiwa na wakulima hao kutoka kwa viongozi wa vyama hivyo.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Blasius Chitanda inaonyesha jumla ya Vyama vya Ushirika 61 bado vinadaiwa na wakulima katika wilaya za Mtwara, Masasi, Tandahimba na Newara kuanzia Msimu wa Korosho wa Mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo baadhi ya wakulima wanaodai fedha zao waliiomba serikali kuhakikisha wanalipwa haki yao kwani madeni hayo yamechukua muda mrefu hali inayopelekea kuzorotesha shughuli zao za kuchumi.

Post a Comment

0 Comments