habari Mpya


Soma Habari ya Saa 24 October 18,2019 Radio Kwizera FM -Ngara.

Source; RK: BF [Takwimu Malaria]
ED: AG
Date: Friday, October 18, 2019

NGARA

Maambukizi ya ugonjwa wa malaria wilayani Ngara Mkoani Kagera yamepanda kwa mwezi Septemba mwaka huu,2019 kwa asilimia 50.1 ukilinganisha na mwezi Agosti ambapo yalikuwa ni asilimia 49.1.

Akizungumza na redio kwizera Mratibu wa Malaria wilaya ya Ngara, Dkt.Madina Kibiriti amesema kiwango cha ugonjwa kimeonekana kupanda kila mara kutokana na wananchi kushindwa kutumia vyandarua na kufuata sheria za usafi.

Dkt. Madina amesema matumizi ya vyandarua kwa wananchi ni asilimia 85 kwa takwimu za Mwaka jana 2018, zilizopatikana wakati wa unyunyiziaji wa dawa ya ukoko majumbani kuanzia mwazi Oktoba hadi Disemba.

Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wilayani Ngara wamesema wamekuwa wakijikinga na ugonjwa huo hasa kwa kufanya usafi wa Mazingira ikiwemo kufukia madimbwi katika sehemu zao za Makazi na kutumia vyandarua jambo ambalo limekuwa likipelekea kuishi salama.

Source; RK: Faraja,M (Upepo)
ED: AG
Date: Friday, October 18, 2019

KAHAMA

Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kumkamata na kumhoji Diwani wa Kata ya Kashishi halmashauri ya Msalala Bw. Samweli Magema kwa tuhuma za kumuoa binti mwenye miaka 19 aliyekuwa akisoma kiato cha pili katika shule ya Sekondari Bulige.

Mkuu wa wilaya ya Kahama Bw. Anamringi Macha amesema taarifa za Diwani huyo kuishi kinyumba na Mwanafunzi huyo kwa zaidi ya wiki mbili, zimetolewa October 17,2019 na Wananchi wa kijiji cha Mwambuko.

Bw. Macha amesema baada ya kupata taarifa hizo waliamua kwenda nyumbani kwa Diwani Magema majira ya saa moja usiku ambapo walimkuta binti huyo na kumchukua hadi kituo cha Polisi kwa uchunguzi zaidi huku wakiacha taarifa za kumtaka Diwani huyo ajisalimishe Polisi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Kashishi Bi. Sophia Yusuphu amesema baada ya kuzipata taarifa hizo waliamua kutoa taarifa ngazi ya wilaya kwa hatua zaidi na kwamba kumekuwepo na matukio mengi ya wanafunzi wa kike kukatisha masomo na kwenda kuolewa.

Source; RK: Gmika (RADI)
ED: AG
Date: Friday, October 18, 2019

GEITA

Wanafunzi 39 wa shule ya Ihumilo kata ya Nkome Mkoani Geita wamenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na radi wakati wakiwa darasani.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita Dkt. Japhet Simeo amesema wanafunzi watatu kati yao wanaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo kata ya Nzera, Wanafunzi 21 wameruhisiwa kurudi nyumbani baada ya afya zao kuimarika huku wengine 15 waliofikishwa katika zahanati ya Nkome wametibiwa na kuruhusiwa.

Hata hivyo, Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Geita Bw.  Kaitila Mrusuli amesema majeruhi hao watatu waliolazwa katika hospitali hiyo wanaendelea vizuri na kwamba muda wowote wataruhusiwa kurudi nyumbani.

Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robart Gabriel amesema serikali inaendelea kuangali njia nzuri ya namna ya kuweka tahadhari ya radi katika majengo yote ya serikali ili kuepusha ajali za radi.


Source; RK: Sam M. (mimba mashuleni)
ED: AG
Date: Friday, October 18, 2019

KAKONKO

Serikali wilayani Kakonko Mkoani Kigoma kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali yajipanga kukomesha tatizo la mimba mashuleni kwa kuwapatia wananfunzi elimu ya afya ya uzazi

Akiongea na Redio Kwizera kupitia Bonanza la Michezo kwa kuwakutanisha Wanafunzi kutoka shule mbali mbali za Sekondari, Mratibu wa Afya ya Uzazi Shule za Sekondari wilayani humo Bw. Majaliwa Tryphone amesema lengo kuu ni kuhakikisha vijana hao wanakuwa na uelewa wa namna ya kujikinga na mihemko ya mwili wakiwa bado wako shuleni

Aidha amesema baada ya kuanza kwa mabonanza hayo kwa kushirikiana na Shirika la World Vision, tatizo la mimba shuleni limepungua hivyo ni jukumu lao kuendelea kukabiliana na tatizo hilo.

Nao baadhi ya Wanafunzi wilayani Kakonko wamesema elimu ambayo wamekuwa wakipatiwa imewasaidia kutambua haki zao na kutokubali baadhi ya vitendo vya unyanyasaji ikiwemo ukeketaji kwa watoto wa kike kutoka kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini.

Source; RK: wm (matokeo)
ED: AG
Date: Friday, October 18, 2019

BIHARAMULO

Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kupitia idara ya elimu msingi imesema imepokea matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa furaha kubwa baada ya kushika nafasi ya tisa kitaifa na nafasi ya pili kimkoa ikitanguliwa na manispaa ya Bukoba.

Afisa Elimu Taaluma  wilaya ya Biharamulo Bw. Amos  Nyamutela amesema hayo wakati akiongea na Radio Kwizera  baada ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani darasa la saba kitaifa na wilaya ya Biharamulo ikawa ndani ya shule  kumi bora  kitaifa zilizofanya vizuri katika matokeo hayo.

Amesema ushindi huo wa awamu ya saba mfululizo umetokana na jitihada za Walimu, Wanafunzi na Wazazi katika kushirikiana mambo mbalimbali ikiwemo ufundishaji, na jitihada za wazazi katika kutimiza wajibu wao kwa kuwapatia vifaa vya shule

Nao baadhi ya Walimu Wakuu wa Shule za msingi Wilaya ya Biharamulo, wamesema ushindi huo umeiletea heshima wilaya ya Biharamulo na shule za msingi na kwamba jitihada hizo zitaendelea ili kuhakikisha wilaya inashika nafasi ya kwanza kitaifa katika miaka ijayo.

Post a Comment

0 Comments